Ibada hii ya kutawazwa huleta pamoja familia za warani pamoja na wenyeji na maafisa wa ndani, katika maelfu ya watu wote. / Picha : Mtandao wa Gavana wa Narok 

Huku wakiwa na tabasamu zito, nywele zao zilitiwa rangi nyekundu na kupambwa kwa vazi la sherehe la manyoya ya mbuni, vijana wa Kimasai 'wako bisee' na kupiga picha za selfie.

Wamemaliza siku ya kwanza ya Eunoto, ibada ya kitamaduni inayoashiria mabadiliko kutoka kwa shujaa yaani 'Mrani' hadi kuwa mtu mzima.

"Leo tunakuwa wanaume," mwanafunzi wa udaktari Hillary Odupoy mwenye umri wa miaka 22 anasema kwa majigambo, akiwa amevalia miwani ya jua na msururu wa lulu kifuani mwake wazi.

Wakiwa na umri wa kati ya miaka 18 na 26, vijana hao walifika kwa mamia katika kijiji cha Nailare kusini-magharibi mwa Kenya, wote kutoka kizazi kimoja cha "warani" ("wapiganaji" katika lugha ya Kimasai), hadhi ambayo wameshikilia kwa muongo mmoja.

Katika hafla ya Enkipaata vijana hutawazwa kutoka ujana hadi hadhi ya moran, sherehe ya Eunoto, tawazo la kuwa "mtu mzima ", na hatimaye Olng'esherr anaashiria mwanzo wa hali ya wazee. / Picha Mtandao wa Gavana wa Narok 

"Ni moja ya sherehe kubwa tulizonazo maishani mwetu. Hatuwezi kamwe kukutana kwa idadi kubwa ya umati kama huu. Inaunganisha jamii ya Wamasai," anaelezea Odupoy.

Kuunganisha jamii

Wote wanavaa nyekundu, rangi takatifu ya Wamasai -kutoka kwa nywele zao ambazo zimepakwa mchanganyiko wa udongo yaani ocher na mafuta hadi shuka zao za kitamaduni.

Ibada hii ya kutawazwa huleta pamoja familia za warani pamoja na wenyeji na maafisa wa ndani, katika maelfu ya watu wote.

Kwa siku tano, sherehe ya Eunoto huangazia nyimbo za kitamaduni za kishindo, densi za faili moja kwenye mguu mmoja, na adumu - mruko maarufu wa Kimasai.

Ng'ombe huchinjwa na damu yao hunywewa na vijana, ambao nywele zao hunyolewa na mama zao.

Kisha wanaachana na upanga wa mashujaa na kupokea fimbo ya kutembea ya "wazee".

Taratibu zilizoachwa

Kwa karne nyingi, wanaume wa Kimasai wamepitia taratibu tatu za kutawazwa ambazo zimeandikwa tangu 2018 kwenye orodha ya UNESCO ya turathi zisizoshikika na zinazohitaji uhifadhi wa dharura.

Kinadharia, vijana wa Kimasai wanaweza kuoa tu baada ya kutawazwa kupitia hafla ya Eunoto,/ Picha : Mtandano wa Gavana wa narok.

Enkipaata ni mpito kutoka ujana hadi hadhi ya moran, Eunoto, tawazo la kuwa "mtu mzima ", na hatimaye Olng'esherr anaashiria mwanzo wa hali ya wazee.

Lakini mila kama hizo za Wamasai, ambao asili yao ni wafugaji wa kuhamahama wanaoishi kusini magharibi mwa Kenya na kaskazini mwa Tanzania, zimelazimika kuendana na mabadiliko na mahitaji ya maisha ya kisasa.

Warani hawatumwi tena kukaa miaka miwili jandoni , lakini hukutana huko wakati wa likizo ya shule ili kujifunza historia na mila za Wamaasai, pamoja na kanuni za maisha katika jamii.

Kufundishwa maadili

"Mbali na kuwa na elimu ya Magharibi, elimu ya jadi pia ni muhimu," anasema mwanafunzi wa kilimo Peter Ledama Ntuntai, 24.

"Utamaduni wetu unatufundisha tabia njema."

Olerina Karia ni mmoja wa wazee wanaofundisha somo hili la maisha kwa vijana wa Kimasai.

"Tunawafundisha kuwa raia wanaowajibika na wanajamii," anasema Karia mwenye umri wa miaka 52.

“Lakini mila zote ambazo hazikuwa bora kwa maisha ya jamii yetu mfano kuua simba au tohara kwa watoto wa kike tunawafundisha kuziacha hasa zikigongana na sheria.

Wamasai ni kundi la 10 kwa ukubwa nchini Kenya na idadi ya watu chini ya milioni 1.2, kulingana na sensa ya mwisho ya 2019/ Picha : AFP

Mauaji ya simba yalikuwa ni kuthibitisha ushujaa wa watu wa Kimasai, lakini imekuwa kinyume cha sheria nchini Kenya kwa miongo kadhaa ili kumlinda mnyama ambaye yumo hatarini kutoweka.

'Ushawishi wa jamii umebadilika'

Kinadharia, vijana wa Kimasai wanaweza kuoa tu baada ya Eunoto, ambapo kizamani bibi harusi alitakiwa awe amefanyiwa tohara.

Lakini tohara ya wanawake, (FGM) imepigwa marufuku nchini Kenya tangu 2011.

"Unaweza kuwa Mmasai bila kuua simba na bila kupitia ukeketaji," anasema Hillary Odupoy.

Siku hizi, baadhi ya morani hawangojei hafla ya Eunoto kabla ya kufunga ndoa.

“Mienendo ya jamii imebadilika, wakienda shule wakati mwingine wanakutana na wachumba wao huko wanafunga ndoa,” anasema Olerina Karia.

Kwa wengi, ni suala la kuishi kuhifadhi mila na utamaduni wa makabila 45 maarufu zaidi ya Kenya.

Wamasai ni kundi la 10 kwa ukubwa nchini Kenya na idadi ya watu chini ya milioni 1.2, kulingana na sensa ya mwisho ya 2019.

"Ni hofu yetu kubwa kwamba katika siku za usoni tunaweza kushindwa kutekeleza utamaduni huu," anasema Olerina Karia.

"watu wengine hata kutok anje ya jamii yetu wameugeuza utamaduni wetu kuwa biashara, wakati wamiliki halisi ambao wanajua jinsi ya kuutunza wanakosa kufaidika nao."

AFP