KAA ilisema timu za kukabiliana na moto zilidhibiti moto huo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) na hakuna majeruhi walioripotiwa./ Picha : Reuters 

Mamlaka ya Viwanja vya Ndege vya Kenya (KAA) imetangaza kufungua tena sehemu ya kupokea ndege za safari za kimataifa Terminal 1E katika uwanja wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi kufuatia kufungwa kwake mapema Jumatatu baada ya kisa cha moto kisichokuwa na majeruhi.

Moto huo unadaiwa kutokana na hitilafu ya umeme na hakuna majeruhi wala uharibifu mkubwa ulioripotiwa.

Hata hivyo kutokana na sababu za kiusalama, Mamlaka ya KAA ililazimika kufunga kwa muda eneo hilo na kuhamisha ndege zote zinazotua kwa sehemu tofauti ya uwanja huo.

"Mbali na taarifa yetu ya awali, tuna furaha kutangaza kwamba Kituo cha 1E (T1E) katika JKIA sasa kinafanya kazi kikamilifu," shirika hilo lilisema katika taarifa yao Jumatatu mida ya alasiri.

KAA ilisema timu za kukabiliana na moto zilidhibiti moto huo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) na hakuna majeruhi walioripotiwa.

Hii sio mara ya kwanza kw amoto kutatiza shughuli katika uwanja wa ndege wa JKIA. Agosti 7 2013, moto mkubwa ulitokea katika sehemu kubwa ya abiria wanaowasili na kusababisha ndege zote zinazoingia nchini kuhamishwa kutua viwanja vingine kama Mombasa au hata nchi jirani Uganda na Tanzania.

TRT Afrika