Tembo wa msituni hukaa kwenye misitu minene ya kitropiki ya Afrika magharibi na kati / Picha: AP

Na Coletta Wanjohi

Istanbul, Uturuki

Afrika ina tembo aina mbili.

Wale tembo wa kawaida tunawaona katika hifadhi na mbuga za wanyama pori wanaoitwa tembo wa savana.

Lakini kuna aina nyengine ya tembo wanaoitwa tembo wa msituni. Tembo wa msituni hukaa kwenye misitu minene ya kitropiki ya Afrika magharibi na kati.

Wanapatikana, nchini Gabon na Jamhuri ya Congo, na idadi ndogo imesalia katika nchi nyingine za Afrika kama Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Equitorial Guinea. Pia wapo Côte d'Ivoire, Liberia, na Ghana katika Afrika Magharibi.

Tembo wa msituni wa Kiafrika ni takriban nusu ya ukubwa wa idadi ya tembo wa kawaida wa savanna na meno yao yamenyooka na yanaelekea chini ikilinganishwa na meno ya nje ya tembo za Savanna iliyopinda.

Madume, au mafahali, wanaweza kuwa na pembe ambazo karibu kugusa ardhini. Masikio ya tembo wa msitu pia yana umbo la mviringo zaidi, kinyume na masikio yenye pembe tatu ya tembo wa savanna.

Tembo wa Savannah huwa katika hifadhi na mbuga za wanyama pori /picha Wengine 

Pia kuna tofauti ya tabia kati yao.

Makundi ya tembo wa msituni wa Kiafrika huwa ni madogo zaidi, na tembo wachache tu katika kila kitengo,

Kwa upande mwingine, tembo wa savanna wa Kiafrika huunda kundi makubwa ambayo yanaweza kuanzia 10 hadi vikundi vya familia zenye tembo 70 au zaidi.

Tembo huyo wa msituni anajulikana kama shujaa wa hali ya hewa. Tembo hula zaidi ya kilo 180 ya chakula kwa siku, hivyo hutumia muda mwingi kutafuta chakula.

Makundi ya tembo wa msituni wa Kiafrika huwa ni madogo zaidi ya wale tembo wa savannah / Picha: AFP

Kwa vile wanyama hawa hupita msituni wakila, hufanya uharibifu mkubwa ikiwemo kukanyaga, kung'oa na kukata majani na mimea inayowazunguka.

Hii inapunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa mimea, hasa miti midogo, ambayo ina msongamano mdogo wa kaboni. Ushindani mdogo wa maji, mwanga na nafasi hutengeneza nafasi kwa ukuaji wa miti mikubwa, inayokua polepole, miti minene na matawi ambayo huunda mianzi mirefu na mipana.

Tembo wa msituni wanakula matunda kwa wingi. Wakishameza matunda tembo hutawanya mbegu kupitia njia ya haja kubwa. Kinyesi chao husaidia kurutubisha mbegu wanazodondosha na hapo kufanya miti muhimu kuendela kukua katika sehemu tofauti misituni.

Wataalamu wanadai kuwa, iwapo ndovu watapokea kabisa msituni, hifadhi ya kaboni iliyo juu ya ardhi katika makazi yao ya misitu ya Kiafrika ingepungua kwa asilimia 7.

Tembo wa msituni wanakula matunda kwa wingi, wakishameza matunda tembo hutawanya mbegu kupitia njia ya haja kubwa. Picha AFP 

Tembo wa msituni wanaweza kuisha mpaka miaka 60 hadi 70 na hukomaa polepole. Wana kiwango cha chini cha uzazi kuliko tembo wa kawaida wa Savanna.

Wanaweza kujamiiana mwaka mzima, lakini shughuli za kilele hutokea wakati wa msimu wa mvua kati ya Oktoba na Mei. Kuelekea kipindi hiki, tembo wa kiume hupata ongezeko la viwango vya testosterone au homoni za kiume —hadi mara sita zaidi ya kawaida.

Hali hii inaweza kudumu miezi miwili hadi mitatu.

Wakati huu, tembo wa kiume huwa wakali sana na wanaweza kuwa hatari kwa watu na wanyama wengine wanaowazuia.

Kasi ya tembo wa msituni kuzaa ni ndogo, kwa sababu wanafuga ndama wapya kila baada ya miaka mitatu hadi sita/ Picha AFP 

Tembo wa kike hubeba mimba kwa takriban muda wa miaka miwili. Huu ndio muda mrefu zaidi kwa mnyama kubeba mimba.

Na kama ilivyo kwa tembo wa Savanna, tembo wa msituni wa Kiafrika kasi yao ya kuzaa ni ndogo, kwa sababu wanafuga ndama wapya kila baada ya miaka mitatu hadi sita.

Idadi ya tembo wa msituni wa Afrika haijulikani kwa sababu wanapenda kukaa katika misitu minene ambayo inafanya zoezi la kuwahesabu kuwa ngumu.

Idadi yao kwa kawaida inakadiriwa kupitia "hesabu za kinyesi"chao kilichosambaa. Lakini fahari hii ya Afrika iko hatarini kutoweka.

Tembo wa msituni wanaendelea kukabiliwa na vitisho. Hii inachangiwa na vitendo vya ujangili wa biashara haramu ya kimataifa ya pembe za ndovu, lakini pia kutokana na upotevu wa makazi yao ya misitu.

Idadi ya tembo wa msituni inaripotiwa kupungua kwa zaidi ya asilimia 86 katika kipindi cha miaka 31.

Wataalmau wanasema kulinda tembo wa misitu na misitu wanayoitegemea inamaanisha tunalinda michango yao ya kiikolojia ambayo sote tunaitegemea.

TRT Afrika