Kenya imezindua mpango wa kukabiliana na migogoro kati ya binadamu na wanyamapori itakayotoa fidia ya hadi shilingi milioni tatu kwa watakao athiriwa na shambulio la wanyama pori.
Akizindua mpango huo, Rais William Ruto alisema hii ni kwa lengo la kuwasaidia kujenga upya maisha yao na kumudu gharama za matibabu.
''Mnajua tumebadilisha sheria sasa. Zamani mtu akiuawa na ndovu alikuwa analipwa shilingi elfu mia mbili, tumesema kama serikali sasa, mwananchi akiuawa na ndovu au mnyama yeyote, tunamlipa shilingi milioni tano,'' alisema Rais Ruto. '' Lakini tumegawanya kwa viwango, wale watakao jeruhiwa wengine watalipwa milioni tatu, wengine milioni mbili, kama amekuumiza zaidi tunafikisha milioni nne,'' aliongezea Rais.
Rais aliendelea kufafanua kuwa visa vya kuumwa na nyoka pia watajumuishwa katika mpango huo.
Ruto aliwaagiza maafisa wa wizara husika kuhakikisha malipo ya fidia hizi zinatolewa ndani ya siku sitini kuanzia tamko lake, ambapo serikali inasema kuna visa takriban 7000 vilivyo chunguzwa na kuhakikiwa, zitakazogharimu shilingi Bilioni tatu kufidiwa.
''Kawaida mwananchi akipata tatizo, safari ya kupata fidia inakuwa safari ngumu sana,'' alisema Rais Ruto. '' Lakini sasa tumeweka mtandao wa pamoja ambao utarahisisha kuripoti, kukaguliwa na hatimaye kuhakiki na kulipwa fidia kwa waathiriwa,'' Rais Ruto aliongezea.
Ujenzi wa ua kulinda mbuga nahifadhi za wanyama
Serikali ya Kenya inasema imechukua hatua hii ili kurudisha imani ya wananchi wanaoishi kando kando mwa mbuga au hifadhi za wanyama, ili washirikiane nao kuhifadhi wanyama pori kama rasli mali ya taifa.
Kati ya miradi nyingine iliyozinduliwa ni ujenzi wa ua kuzunguka mbuga zote za taifa na hifadhi za wanyama ili kuwalinda binadamu na wanyama pia.
Rais Ruto alisema kuwa mradi huu utapanuliwa kwa kaunti sita zinazochangia mbuga na hifadhi za wanyama nchini Kenya kwa maeneo yote hayo yanakumbwa na visa vya mara kwa mara vya mzozo kati ya binadamu na wanyama pori.
''Ndani ya miaka mitano ijayo, lazima tuwe tumehitimisha shughuli ya kuweka ua kwa mbuga zote na hifadhi za wanyama nchini, ili tupunguze tatizo hili l amizozo kati ya wanyama pori na binadamu,'' ameendelea kusema Rais Ruto.
Serikali ya Kenya imesema imepokea visa 17000 vya watu waliojeruhiwa au kuuawa na wanyama pori, ambavyo vimeshathibitisha. Visa hivi vitaigharimu serikali jumla ya zaidi ya shilingi Bilioni 7 kufidia, ambapo visa 10000 tayari vimelipwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 4. Sasa Rais ameagiza wale 7000 waliosalia walipwe fidia zao ndani ya siku sitini zijazo.