Eudes Ssekyondwa
TRT Afrika, Kampala, Uganda
Kwa mwaka wa 8 sasa, Amos Wachira amewekeza muda wake na utaalamu wake katika kuchakata vioo na chupa zilizotupwa na kuwa vitu vya thamani.
TRT Afrika ilipokutana naye katika kiwanda chake jijini Kampala nchini Uganda, alikuwa akitoa maelezo kwa mfanyakazi wake mmoja ambaye anasema bado anaendelea kujifunza.
"Kwa sasa ninawafundisha watu wanne kupata utaalamu huu," anaimbia TRT Afrika,"Inahitaji uvumilivu mwingi kwani tunafanya kazi ya kuchosha."
Ndani ya kiwanda hicho, joto ni kali. Hata hivyo, Wachira na wasaidizi wake wanne wanaonekana kuzoea mazingira hayo. Wakiwa katika nguo zao za kazi, maarufu 'ovaroli' na vifaa vya usoni vya kuwakinga, jasho linawatiririka mwilini.
"Hebu angalia hiyo kioo isiharibike katika hiyo moto," Wachira anatoa maelezo kwa msaidizi wake, huku naye akichukua kile ambacho anatuelezea ni kipuliza joto.
Hii ni fimbo ya chuma ambayo inatumika kutoa maumbo tofauti katika kioo kilichoyeyushwa.
"Kazi yetu huanza kila siku mitaani, kwa kuokota vioo na chupa," Wachira anaielezea TRT Afrika,"Mtu anaweza kuona kama ni kazi chafu, lakini huo uchafu ndiyo msingi wa utaalamu wetu."
Uchafu mitaani
Ukitembea katika mitaa ya Kampala, si vigumu kuona vioo vilivyotupwa kiholela sehemu tofauti.
Vioo vinachangia kwa asilimia kubwa katika sekta ya ujenzi nchini Uganda huku makampuni mengi hasa ya vinywaji yakiweka bidhaa zao katika chupa. Baada ya fundi kupima vioo wanayotaka yale machepechepe yaliyobaki hutupwa.
"Mifumo yetu ya kusafisha jiji haina ujuzi maalumu wa kuondoa vioo na chupa katika mazingira, na mikakati ya jumla ya kuondoa takataka," anasema Jude Byansi Ziwa, Meneja wa Halmashauri ya jiji la Kampala, KCCA.
Hivyo kumekuwa na juhudi zaidi za kuondoa plastiki kutoka katika mazingira na kuziongezea thamani kuwa vitu bora, ingawa jitihada zinazoelekezwa katika vioo na chupa si nyingi.
"Watu wetu tumewaambia wakusanye uchafu hii wasitupe kwenye mazingira au hata wakusanye mahala salama," anasema Ziwa," Mara nyingi tunaamini kuwa kile ambacho hakirudishwi tena siku za usoni kitatumika tena na kutumika kama rasilimali,"
Jitihada kama za Wachira zinakuja kutoa suluhu kwa changamoto hii.
"Niliitwa hapa mwaka wa 2016 na kampuni moja wa Uganda ambayo ilitaka kuanzisha mradi huu," Wachira anaielezea TRT Afrika, "Tulianza mradi huu katika mji jirani wa Mukono na huko tayari umefanikiwa."
Hapa jijini Kampala, ana wanafunzi wanne.
"Tayari watu wawili wameelewa kabisa kazi hii na ninaweza kuwaita wataalamu, wamebaki hawa wawili, lakini wanaonyesha kuelewa kwa kasi," anatuambia huku akiendelea kutoa maelezo.
Kuchakata kioo na chupa
Baada ya kuokota vioo na chupa kutoka mitaani, kawaida zinakaguliwa na kutenganishwa, kati ya zile zinazofaa na zisizofaa.
Halafu vinawekwa katika tanuri lenye moto mkubwa kwa jili ya kuviyeyusha.
Hii inawezakuchukua muda wa saa tatu.
Baadaye Wachira anapuliza hewa katika kioo kilichoyeyushwa na hapo kumwezesha kupata umbo la vyombo tofauti.
Bidhaa hizi baadaye, kwa umaridadi huingizwa sokoni na kuuzwa. Unaweza usiamini ukimbiwa zinatokana na vioo vitokanavyo na takataka.
Umuhimu wa kuchakata kioo na chupa
Ingawa uchafuzi wa mazingira utokanao na plastiki ndiyo umekuwa ukipewa kipaumbele, uchafu wa vioo pia ni changamoto kubwa,
Shirika la Umoja wa Mtaifa linalohusika na mazingira, UNEP linasema kuwa zaidi ya 90% ya taka zinazozalishwa Afrika, zinatupwa kwenye sehemu zisizodhibitiwa na mara nyingi kuchomwa wazi.
Wataalam wa mazingira wanasema kiwango cha kimataifa cha kuchakata glasi kinakadiriwa kukaribia 21%.
Hii ina maana kwamba kwa kila tani 100 za vioo zinazozalishwa, ni tani 21 pekee zinazorudishwa na kupata thamani upya, huku tani 79 zilizosalia zikitupwa ardhini au kuchomwa moto.
"Kioo kinachozalishwa kutoka katika glasi iliyorejelewa na kupewa thamani hupunguza uchafuzi wa hewa unaohusiana kwa asili mia 20% na uchafuzi wa maji unaohusiana na 50%," inasema Shirika la WorldWide Fund, WWF.
Wachira anasema katika nchi yake ya asili, Kenya, kuna ujuzi mwingi wa kuchakata vioo na chupa zilizotupwa. Hivyo baada ya kuwafunza watu Uganda hunda akaelekea katika nchi nyengine ambazo bado zina hitaji ujuzi huu wa kuokoa mazingira.