Na Coletta Wanjohi
Istanbul, Uturuki
Kabla ya kuanguka mwaka wa 2018, mbuyu mkubwa unaojulikana kama 'Tsitakakoike' ulifahamika kama mbuyu mkubwa zaidi duniani. Ulikuwa na upana wa mita 27 na umri wa miaka 1400.
Fahari hii ilikuwa nchini Madagascar. Madagascar ni kisiwa kando ya pwani ya Msumbiji katika Bahari ya Hindi.
Mibuyu pia inaota katika nchi nyengine 31 za Afrika zikiwemo zile za nchi za Afrika Mashariki.
Ukisafiri Tanzania, mibuyu ya aina tofauti utakayoina pale kaskazini mwa Mbuga ya Taifa ya Tarangire.
Nchini Kenya, mbuyu una thamani kubwa hasa katika jamii ya maeneo ya watu wa pwani, huku baadhi wakiitambua kama sehemu ya kufanyia matambiko.
Lakini nchini Madagascar, mti huu hukuwa kwa wingi na kwa ukubwa wa kustaajabisha. Kati ya spishi 9 za mbuyu duniani, sita ziko Madagascar pekee.
Ukiwa Madagascar, hasa magharibi mwa nchi utashuhudia mibuyu mikubwa. Mbuyu pia unajulikana kama "mti ulioinama chini.
"Wenyeji hapa wana simulizi tofauti.
Baadhi wanadai kuwa mbuyu hapo zamani ulikuwa mti wa fahari, lakini uliadhibiwa na miungu kwa ubatili wake. Kwamba mti uling'olewa na kupandwa kichwa chini kama ukumbusho wa kiburi chake. Hizi ni hadith za jamii zetu.
Mbuyu unaweza kuishi zaidi ya miaka 3000 na kufikia urefu wa mita 30 na mzunguko wenye upana wa mita 50.
Wataalamu wanasema una uwezo wa kuishi katika mazingira magumu na yenye ukame kutokana na uwezo wake wa kuhifadhi kiasi kikubwa cha maji kwenye shina lake. Kwa wananchi wa Madagascar, mbuyu si mti tu, umekita mizizi katika utamaduni za Kimalagasi.
Mbuyu pia ni ishara ya unyenyekevu na ustahimilivu. Mti huu hutoa matunda ya kipekee ambayo hukauka kiasili kwenye tawi lake.
Badala ya kudondoka na kuharibika, hubaki kwenye tawi na kuoka juani kwa muda wa miezi 6 - na kubadilisha rangi yake ya kijani kibichi na kuwa ganda gumu kama nazi. Massa ya matunda hukauka kabisa.
Hii ina maana kwamba tunda linahitaji kuvunwa, kukatwa na kuchujwa ili kutoa unga wa tunda safi.
Yale mabuyu au ubuyu unaopenda kumumunya ukiwa katika rangi nyengine au manjano, unatoka katika mti huu.
Pia hutumika kutengeneza vipodozi. Gome la mbuyu ni muhimu kwa kutengeneza kamba, nguo na vikapu.
Mti huu pia hutumika kutengeneza dawa za kienyeji zinazotibu magonjwa mbalimbali kama vile homa na kuharisha.
Kwa kuongezea, mbuyu pia hutumika kutengeneza ala za muziki na kujenga nyumba. Inaripotiwa wakati wa jadi, watu walitegemea miti hii wakati wa ukame pindi mito ilipoanza kukauka na mvua kuadimika.Kwani mbuyu mmoja unaweza kuwa na lita 4,500 ya maji ndani yake.
Hata hivyo, fahari hii ya Madagascar ipo hatarini kutoweka.Mabadiliko ya hali ya hewa, ukataji miti, vyote vinaiweka mibuyu hatarini.
Miti kadhaa ya mibuyu nchini Madagascar pia imeharibiwa na Kimbunga Enawo, dhoruba kali iliyopiga kisiwa hicho mwaka wa 2017.
Wataalamu wanasema kuna haja ya kuweka juhudi zaidi ili kuhifadhi miti hiyo ambayo Afrika, inafahamika kama miti ya maisha.