Taswira ya kimbunga Ialy, kama kinavyoonekana katika picha za satelaiti./Picha: TMA

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa ya uwepo wa kimbunga “IALY” katika Bahari ya Hindi kaskazini mwa kisiwa cha Madagascar.

Katika taarifa iliyochapishwa katika tovuti yake Mei 17, 2024, TMA imesema kuwa mifumo ya hali ya hewa inaonesha kuwa kimbunga hicho kitaendelea kusalia katika Bahari ya Hindi katika eneo kati ya Madagascar na visiwa vya Shelisheli kwa siku nne zijazo kabla ya kuanza kupungua nguvu.

Hata hivyo, TMA imeondoa hofu ya athari ya kimbunga IALY kutokana na sababu za umbali.

"Kutokana na umbali kutoka nchini, kimbunga hicho hakitarajiwi kuwa na athari za moja kwa moja katika kusababisha ongezeko la mvua nchini. Hata hivyo vipindi vya upepo mkali na mawimbi makubwa vinaweza kujitokeza katika Bahari ya Hindi," imesomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Vile vile, mamlaka hiyo imesisitiza kuwa itaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga hicho na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila inapobidi.

Kimbunga Hidaya kilisababisha mvua zilizonyesha kwa saa 36, zikiambatana na upepo mkali na kusababisha vifo vya watu watano na majeruhi saba, huku kaya 7,027 zenye watu 18,862 zikiathiriwa.

TRT Afrika