Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO limeitambua Hifadhi ya Taifa ya Nyungwe, nchini Rwanda na kuiweka katika orodha ya Urithi wa Dunia.
Hifadhi hii ya Kitaifa ya Nyungwe, ipo katika mkoa wa kusini na magharibi mwa Rwanda.
" Kuorodheshwa huku kutafungua hatua muhimu katika kuhakikisha uhifadhi wake wa muda mrefu, kuhifadhi urithi wake wa asili kwa vizazi vijavyo, na kukuza maendeleo endelevu kwa jamii jirani," Tume ya Maendeleo ya Rwanda, imesema katika taarifa yake.
Utajiri wa Eneo la Hifadhi la Nyungwe
Eneo hili ni mojawapo ya misitu mikongwe zaidi barani Afrika na ni la kwanza nchini Rwanda kutambuliwa na Shirika la UNESCO.
"Kutambuliwa eneo hili letu la Hifadhi sio tu mchango katika kuhifadhi urithi wa asili wa Rwanda, lakini pia ni muhimu sana kwa wananchi wa Rwanda," waziri wa Umoja wa Kitaifa na Ushirikiano wa Kiraia, Jean Damascene Bizimana alisema
Bizimana yuko Riyadh nchini Saudi Arabia ambapo kamati ya UNESCO inafanya mkutano wake ulioanza tarehe 10 na kutarajiwa kumaliza 25 Septemba mwaka huu.
Eneo la Mbuga ya wanyama ya Nyungwe ni msitu mkubwa wenye mvua ambao unachukua hadi hekta 101,900. Eneo ili linalisha mito miwili mirefu zaidi duniani - Mto Nile na Mto Kongo - na ni chanzo cha hadi asilimia 70 ya maji safi ya Rwanda.
Kulingana na taarifa ya Tume ya Maendeleo ya Rwanda, msitu huo ulioanzishwa kama hifadhi ya asili mwaka wa 1933 ukawa hifadhi ya taifa mwaka 2005 katika jitihada za Serikali za kuimarisha ulinzi wake na kulinda maelfu ya wanyama walio katika hatari ya kutoweka na wanaoishi katika mazingira hatari.
Hifadhi ya Taifa ya Nyungwe ina aina nyingi ya viumbe hai, vikiwemo zaidi ya spishi 12 za nyani, aina 322 ya ndege, aina 200 ya maua ya orchid yanayotambulika na karibu aina 300 za vipepeo.