Ripoti ya Umoja wa Mataifa inaonyesha kuwa nchini Ethiopia zaidi ya watoto milioni 9 kwa sasa hawako shuleni kote nchini kwa sababu ya migogoro, vurugu, majanga ya asili, na kuhama makazi yao.
Zaidi ya shule 6,000, zimefungwa na takriban shule 10,000 ambazo ni asilimia 18 ya jumla ya shule, ziliharibiwa kutokana na majanga ya hali ya hewa na migogoro, ripoti hiyo imesema.
Ripoti hii ya Shirika la Umoja wa Mataifa linalotetea watoto, lilifanya ukaguzi wa hadi Novemba 2024.
Ripoti hiyo inaangazia idadi kubwa zaidi ya watoto wasiokwenda shule ambao hupatikana katika mikoa ya Amhara (milioni 4.4), Oromia (milioni 3.2), na Tigray (milioni 1.2).
Hivi majuzi, Taasisi za Elimu ya Juu katika Mkoa wa Amhara ilifichua kuwa watoto milioni 4.7 katika mkoa huo hawaendi shule, na ni 32% pekee waliojiandikisha katika mwaka huu wa masomo.
Katika eneo al Tigray kaskazini mwa nchi, vita kati ya serikali na kikundi cha Tigray Peoples Liberation Front, TPLF, vilikuwepo kati ya 2020 na 2022. Vita hivyo vilipelekea maelfu kupoteza maisha na wengine kuhama makwao na hivyo kuathiri elimu.
Katika eneo la Amhara vita vinaendelea kati ya jeshi la serikali na vikundi vyenye silaha huku ukosefu wa amani ukiwaacha watoto wengi nje ya madarasa.