Shirika la Umoja wa Mataifa limekemea vikali mauaji ya raia katika kambi ya wakimbizi ya Lala mkoani Ituri.
Katika taarifa yao, baraza la usalama la umoja huo lilitaja shambulio hilo ambalo lililenga hususan raia, kuwa uhalifu wa kivita na kutoa wito kwa serikali kufanya uchunguzi wa kina na kuwakamata walio husika.
Shabulio hilo lililotokea Kuanzia Jumapili limesababisha vifo vya watu 45 na kuwajeruhi wengine 10.
Kwa mujibu wa baraza hilo, kundi la wanamgambo wa ushirikiano na maendeleo ya Congo CODECO ndilo lilihusika.
Wasiwasi umetanda kutokana na ongezeko la mashambulio ya makundi ya waasi mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, huku Umoja wa Mataifa ukiyataka makundi yote hasimu kuweka silaha chini na kurejelea mazungumzo na serikali ya kutafuta Amani ya kudumu.
Makundi hayo yamekuwa yakishutumiwa kufanya mashambulio dhidi ya wanawake na watoto huku yakiwateka baadhi ya watoto na kuwaingiza kundini kama wapiganaji.
Kenya inaandaa mazungumzo ya upatanishi ya makundi husika kwa lengo la kuunda azimio la kisiasa litakalo wezesha kuweka silaha chini, kurejesha wakimbizi wa ndani katika jamii zao na kuondolewa kwa makundi ya kigeni yanayopigana ndani ya Congo kurudi nchi walikotokea.