Kwa takriban mwaka mmoja, Haiti, kupitia Umoja wa Mataifa imekuwa ikiomba uingiliaji kati wa kimataifa kusaidia polisi wake Picha :  Reuters

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres Jumatatu alipongeza hatua ya Kenya kuridhia kuongoza kikosi cha kimataifa kusaidia polisi wa Haiti kupambana na ghasia za magenge na kuhimiza nchi nyingine - hasa kutoka eneo la Haiti - kujiunga na jitihada.

Kenya ilisema kuwa iko tayari kupeleka maafisa 1,000 wa polisi kusaidia kutoa mafunzo na kusaidia polisi wa Haiti "kurejesha hali ya kawaida nchini na kulinda mitambo ya kimkakati," Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Alfred Mutua alisema katika taarifa yake Jumamosi.

Kwa takriban mwaka mmoja, Haiti, kupitia Umoja wa Mataifa imekuwa ikiomba uingiliaji kati wa kimataifa kusaidia polisi wake, lakini hakuna nchi yoyote iliyojitokeza kufikia sasa.

Bwana Guterres amesisitiza wito wake kwa Baraza la Usalama kuunga mkono operesheni hiyo ya kimataifa isiyo ya Umoja wa Mataifa na kuhimiza nchi wanachama, haswa kutoka kanda, kuunganisha nguvu na Kenya.

Kwa upande wake Waziri mkuu wa Canada Justin Trudeau aliashairia kuwa wako tayari kusaidia juhudi zozote za kimataifa kupambana na uhalifu Haiti.

"Nimefurahi sana kuona kwamba mataifa mengine mengi yanashiriki kusaidia," Waziri Mkuu wa Kanada Justin Trudeau aliwaambia waandishi wa habari Jumatatu alipoulizwa kuhusu tangazo la Kenya, na kuongeza kuwa alikuwa akiendelea na mazungumzo na Umoja wa Mataifa kuhusu kile Canada inaweza kufanya kwa Haiti. .

Kwa upande wake Serikali ya Haiti imepokea vyema pendekezo la Kenya kutuma kikosi cha polisi ikisema kuwa itasaidia kurejesha utulivu katika nchi ambayo imevamiwa na magenge haramu.

TRT Afrika