Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio la kulaani mashambulizi dhidi ya kitabu kitakatifu cha Waislamu, Qurani, licha ya kura za nchi za Magharibi kupinga azimio hilo.
Rasimu ya azimio hilo iliwasilishwa na Pakistan kwa niaba ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) yenye wanachama 57.
Azimio hilo, ambalo linataka kulaaniwa kwa mashambulizi yanayolenga Quran na kuyataja kama "vitendo vya chuki za kidini," lilipigiwa kura na baraza hilo lenye wanachama 47.
Azimio hilo lilipitishwa huku nchi 28 zikipiga kura ya ndio, nchi 12 zikipinga, na nchi 7 kutoshiriki katika kikao cha kawaida cha 53 cha Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa.
Nchi zilizopiga kura kuunga mkono azimio hilo ni pamoja na Algeria, Argentina, Bangladesh, Bolivia, Cameroon, China, Ivory Coast, Cuba, Eritrea, Gabon, Gambia, India, Kazakhstan, Kyrgyzstan, Malawi, Malaysia, Maldives, Morocco, Pakistan, Qatar, Senegal, Somalia, Afrika Kusini, Sudan, Ukraini, Falme za Kiarabu, Uzbekistan, na Vietnam.
Ubelgiji, Costa Rica, Jamhuri ya Cheki, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Lithuania, Luxemburg, Montenegro, Romania, Uingereza, na Marekani zilipiga kura kupinga azimio hilo.
Uturuki haina haki ya kupiga kura, kwani ina nafasi ya mwangalizi katika Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa.
Pia, Uingereza, Marekani na baadhi ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zilikataa kulaani kuchomwa moto kwa Quran wakati wa mjadala wa dharura Jumanne kwenye Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa.