Marufuku ya kuvaa vazi la uso katika shule za Misri iliyotangazwa na serikali wiki hii imezua mjadala mkali kwenye mitandao ya kijamii Jumanne, huku watu wengine wakidai kuwa ni "udhalimu."
Uamuzi wa Wizara ya Elimu, uliotangazwa katika gazeti la serikali la Akhbar al-Youm siku ya Jumatatu, unahusisha shule za serikali na za kibinafsi.
Marufuku hiyo, inajumuisha niqab ambalo ni vazi jeusi la kiisalmu ambalo huacha tu sehemu ya macho kuonekana na huvaliwa na wanawake wachache nchini Misri.
Uamuzi huo umeacha wanafunzi kuendelea kuvaa hijabu, ambayo ndiyo inayovaliwa na idadi kubwa zaidi ya wanawake.
Uamuzi lazima ufanywe kulingana na "matakwa ya mwanafunzi, bila shinikizo au shuruti kutoka kwa mtu yeyote isipokuwa mlezi wake wa kisheria, ambaye lazima ajulishwe kuhusu chaguo hilo," amri hiyo ilisema.
Watu walijitokeza kwenye mitandao ya kijamii kukemea hatua hiyo, huku wakiishutumu kuingilia masuala binafsi.
"Watu wana hasira kwa sababu serikali haikutoa uhalali wowote. Ni uamuzi wa kidhalimu unaoathiri maisha ya binafsi ya watu," mtumiaji anayejulikana kwa jina la Mohammed alichapisha kwenye X, ambayo zamani ilijulikana kama Twitter.
Hata hivyo, wengine walisema kwamba ni wachache tu wenye itikadi kali ambao wataathirika na uamuzi huo.
"Hakuna aliyekasirika isipokuwa wafuasi wa kundi la Taliban na 'Islamic State'," alichapisha mtumiaji anayejiita "al-Masri" (Mmisri).