Guterres

Umoja wa Mataifa umeeleza wasiwasi wake kuhusu mafanikio ambayo makundi ya kigaidi yanapata katika eneo la Sahel na maeneo mengine ya Afrika.

"Msukosuko wa ugaidi unazidi kuongezeka, huku wapiganaji, fedha na silaha zikizidi kutiririka kati maeneo fulani barani Afrika, na bara zima - na miungano mipya ya ugaidi ikiundwa na uhalifu uliopangwa na vikundi haramu," amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres

Kwa mujibu wa ripoti ya kimataifa ya ugaidi ya 2022 barani Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara ilichangia asilimia 48 ya vifo vya ugaidi duniani, huku eneo la Sahel likitajwa kuwa makazi ya makundi ya kigaidi yanayo semekana kuwa hatari.

Utafiti huu wa ugaidi duniani umefanywa na Taasisi ya uchumi na amani yenye makao yake Australia.

Maeneo yaliyo athiriwa na ugaidi barani Afrika ni pamoja na Somalia, eneo la ziwa Chad, Sahel na sehemu za kusini mwa Afrika.

Boko Haram pia bado ni changamoto katika kutekeleza mauaji, utekaji nyara na vitendo vikubwa vya ukatili dhidi ya raia nchini Nigeria, Cameroon, Chad na Niger.

"Kuna haja ya kuhamasisha rasilimali ya fedha zinazohitajika kwa misheni zinazoongozwa na Umoja wa Afrika kuzuia na kupambana na ugaidi," alisema Azali Assoumani, rais wa Comoros na mwenyekiti wa Umoja wa Afrika.

Umoja wa Afrika umetuma walinda amani nchini Somalia chini ya taasisi ya Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) na kikosi cha pamoja cha kimataifa katika Bonde la Ziwa Chad.

Jumuiya ya maendeleo ya kusini mwa Afrika (SADC) umetuma ujumbe wa kijeshi nchini Msumbiji, tangu Julai 2021, kupambana na ugaidi katika jimbo la Cabo Delgado.

"Kuna haja ya kuzuia itikadi kali za kikatili kupitia kuimarishwa kwa jamii na kuanzisha mfuko wa kifedha wa kuimarisha mipango ya maendeleo endelevu ya kijamii, na hivyo kuzalisha ajira kwa vijana, hasa katika Afrika na Mashariki ya Kati,"

Alisema Filipe Jacinto Nyusi, Rais wa Msumbiji na rais wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa mwezi Machi.

TRT Afrika