Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini amesema nchi hiyo "bado haiko tayari" kufanya uchaguzi wake wa kwanza wa rais katika mwaka ujao.
Nicholas Haysom anasema alishiriki katika "maoni ya wazi" wakati wa mkutano wa Tume ya Pamoja ya Ufuatiliaji na Tathmini nchini Sudan Kusini, Alhamisi.
Haysom anasema maoni yake yanatokana na hisia zilizotolewa na baadhi ya viongozi wa serikali, vyama vya siasa na mashirika ya kiraia kwamba nchi "kwa wakati huu haiko tayari kwa uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika."
Mkuu huyo wa ujumbe wa UN alisema pia hakuna tume ya uchaguzi ulioundwa upya na baraza la vyama vya siasa.
Uchaguzi wa rais unatazamiwa kama ishara kuu ya kutimiza makubaliano ya amani yaliyotiwa saini miaka mitano iliyopita ili kuliondoa taifa hilo changa zaidi barani katika mapigano yaliyoua takriban watu 400,000.
Mazingira ya kisiasa
Haysom alisema ni lazima kuwe na mazingira ya kisiasa na usalama yanayofaa kabla ya uchaguzi kufanywa.
"Sudan Kusini hata hivyo inaweza kupiga hatua kubwa kufikia lengo hili la Desemba 2024 kukiwa na makubaliano ya kisiasa, rasilimali za kutosha na kujitolea kuunda mazingira ya kisiasa yanayofaa," alisema.
Rais Salva Kiir na mpinzani wake aliyegeuka kuwa makamu wake Riek Machar walizozana katika siku za hivi karibuni kuhusu rais kuamua kuwaondoa mawaziri wa ulinzi na mambo ya ndani.
Mkataba wa amani uliotiwa saini mwaka 2018 ulisema kwamba Kiir angemteua waziri wa mambo ya ndani huku Machar ateue waziri wa ulinzi.
Lakini rais amewafuta kazi mawaziri wote wawili.
Kwa kuongezea, nchi bado haijapeleka vikosi vyake vya ulinzi vilivyounganishwa, vilivyoundwa na makundi ya zamani,ikiwa hii ni sehemu ya makubaliano ya amani.
‘Ukosefu wa fedha’
Serikali inasema utumizaji wa maendeleo umechelewa kutokana na ukosefu wa fedha, lakini wataalm wanasema ni kutokana na ukosefu wa nia njema ya kisiasa.
"Wakati ni muhimu kwani vipengele muhimu vya Mipango ya Mpito ya Usalama vinasalia nyuma ya ratiba," Haysom alisema.
Rais Kiir alisema Jumanne kuwa uchaguzi uliocheleweshwa kwa muda mrefu nchini mwake utafanyika mnamo 2024 na amejitosa katika kinyan'ganyiro hiki .
Anatarajiwa kukazania kiti cha urais na Machar, ambaye bado hajathibitisha kugombea kwake.
Upinzani umeishutumu serikali kwa kukosa nia ya kisiasa ya kufanya uchaguzi, lakini Kiir alisema amejitolea kufanya uchaguzi huru na wa haki.