Umoja wa mataifa unasema vita nchini Sudan kati ya jeshi la taifa la Sudan na wapiganaji wa Rapid Support Forces, vimekatiza dalili ya mazungumzo kuendelea kati ya Sudan na nchi jirani ya Sudan Kusini kuhusu mzozo wao wa eneo la Abyei,
Vita Sudan vilianza Aprili 15 mwaka huu.
Eneo la Abyei, ambalo lina utajiri mkubwa wa rasilimali ya mafuta, linapita mpaka kati ya Sudan na Sudan Kusini, na linadaiwa na nchi hizo mbili.
"Pamoja na mzozo nchini Sudan, masharti hayafai kwa mazungumzo kuhusu hali ya hatma ya Abyei. Maendeleo ambayo yalipatikana, mapema mwaka huu, kwa bahati mbaya halikuwa jambo ambalo tunaweza kulijengea,” Hanna Serwaa Tetteh, mjumbe maalum wa katibu Mkuu wa UN katika pembe ya Afrika, aliwaambia mabalozi katika mkutano wa UN wa Baraza la Amani na Usalama.
Baraza la Usalama liliidhinisha kwa mara ya kwanza kikosi cha kulinda amani huko Abyei Juni 2011, wiki chache kabla ya Sudan Kusini kuwa taifa changa zaidi duniani lililo huru.
"Viongozi wakuu wa Sudan na Sudan Kusini hawajaonyesha nia ya kujihusisha na maongezi kuhusu mvutano wao wa eneo la Abyei," aliongeza.
Umoja wa mataifa unahofia kuwa vikosi vya Rapid Support Forces, vinavyopigana na Jeshi la Sudan (SAF) nchini Sudan, sasa vinakaribia Abyei.
"Ubalozi wa Umoja wa Mataifa pia umeshuhudia kuongezeka kwa silaha huko Abyei, hali ambayo inaweza kuwa imechangiwa na hali ya mzozo nchini Sudan," Mkuu wa UN wa operesheni za amani Jean-Pierre Lacroix aliwaambia mabalozi.
"Mgogoro huo pia umesababisha matatizo ya kiuchumi kwa wakaazi wa Abyei kwani bidhaa ambazo nyingi zilitoka kaskazini, zimetatizika."