Wapiganaji wa eneo la Amhara waliunga mkono wanajeshi wa serikali ya Ethiopia kupigana na waasi katika eneo la Kaskazini mwa nchi kati ya 2020 na 2022  / Picha: Reuters

Umoja wa Mataifa unafikiria kusimamisha shughuli za misaada, ikiwa ni pamoja na kuwasilisha misaada ya chakula, katika eneo la Amhara nchini Ethiopia, kufuatia mashambulizi mabaya dhidi ya wafanyakazi wa mashirika ya kibinadamu, kulingana na pendekezo lililoonekana na Reuters na kuthibitishwa na wanadiplomasia wawili.

Wafanyakazi watano wa misaada waliuawa katika miezi sita ya kwanza ya 2024, 10 walipigwa au kujeruhiwa na 11 kutekwa nyara na makundi ya wahalifu wasiojulikana, kulingana na hati ambayo ni ya Agosti 2024.

Amhara ni makazi ya zaidi ya watu milioni 36 pamoja na kituo cha kwanza cha maelfu ya wakimbizi wanaokimbia vita katika nchi jirani ya Sudan.

Mapigano kati ya jeshi la Ethiopia na wanamgambo wa Amhara Fano yalizuka Julai 2023 na yameua mamia na maelfu na wengine kuyahama makazi yao kulingana na makadirio ya Umoja wa Mataifa.

Wanamgambo wa Fano walipigana pamoja na jeshi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka miwili vilivyoikutanisha Addis Ababa na kundi la Tigray People's Liberation Front, ambalo linadhibiti eneo la kaskazini la Tigray.

Waraka huo wa kurasa tatu, ambao umeandikwa "mawasiliano ya ndani," unasema kuwa Umoja wa Mataifa "unazingatia kwa umakini kutekeleza usitishaji wa muda wa shughuli za misaada katika eneo hilo."

Mashirika kadhaa yasio ya serikali na wafadhili tayari wamepinga hatua hiyo, kulingana na vyanzo vitatu vinavyofahamu mjadala unaohusu pendekezo hilo.

Kusitishwa kwa shughuli za usaidizi kunaweza kuathiri zaidi ya watu milioni 2.3 huko Amhara ambao wanategemea msaada wa chakula ili kuishi, mataifa mawili wafadhili na mashirika yasio ya kiserikali yanayopinga yaliiambia Reuters kwa sharti la kutokujulikana.

Wakati wa mzozo huo, serikali ya Ethiopia ilikanusha tuhuma za kutumia njaa kama silaha ya vita dhidi ya Tigray, ambayo ilikuwa chini ya kizuizi.

Baada ya vita kumalizika, uhusiano kati ya Fano na serikali ulivurugika kutokana na shutuma kwamba Addis Ababa ilikuwa inahujumu usalama wa Amhara kwa kulivunja jeshi lake la kikanda.

TRT Afrika