Umoja wa Mataifa, kupitia Baraza lake la Usalama, siku ya Jumatano limeanza mchakato wa miaka miwili wa kuondoa mpango wake wa kulinda amani nchini Somalia maarufu kama UNSOM, baada ya kuwepo huko kwa zaidi ya muongo mmoja.
UNSOM ilianzishwa mwaka 2013 na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuzisaidia mamlaka za Somalia wakati wa safari ya kuelekea utawala wa kidemokrasia na utawala wa sheria baada ya miaka zaidi ya 20 ya mgogoro kati ya wanamgambo na vikundi vya kihalifu.
Kwa sasa, Rais wa nchi hiyo Hassan Sheikh Mohamud bado anatafuta namna ya kuinusuru nchi hiyo kwenye ukosefu wa amani ya kudumu.
Mwezi Mei mwaka huu, serikali yake iliiuomba umoja huo kukamilisha mpango wa UNSOM, ambao unamaliza muda wake mwezi Oktoba. Hata hivyo, ilibadili maombi hayo, ikiomba muda wa miaka miwili wa mpito.
Kukamilika kwa UNSOM
Katika azimio lililopitishwa kwa kauli moja siku ya Jumatano, Baraza la Usalama lilikubali kuendelea na kipindi cha mpito, huku likiazimia kumaliza mpango wa UNSOM ifikapo Oktoba 31, 2026.
Katika mwaka wa kwanza wa kipindi cha mpito, ujumbe huo utazingatia zaidi juhudi za kufanya uchaguzi huru na wa haki, na ulinzi wa haki za binadamu. Baadhi ya majukumu yake yatakabidhiwa kwa mamlaka ya Somalia mwishoni mwa mwaka wa kwanza.