Haikubainika wazi mara moja ukubwa wa kikosi hicho. Awali serikali ya Kenya ilipendekeza kutuma maafisa 1,000 wa polisi.  Picha : AA

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepiga kura kutuma kikosi cha kimataifa nchini Haiti kikiongozwa na Kenya kusaidia kukabiliana na magenge ya kikatili katika nchi hiyo yenye matatizo ya Caribbean.

Azimio hilo lililoandaliwa na Marekani liliidhinishwa kwa kura 13 za ndio na mbili hazikushiriki.

Azimio hilo linaidhinisha kikosi kutumwa kwa mwaka mmoja, na kufanyiwa mrejesho baada ya miezi tisa.

Itakuwa ni mara ya kwanza kwa kikosi hicho kutumwa Haiti tangu ujumbe ulioidhinishwa na Umoja wa Mataifa karibu miaka 20 iliyopita.

Tarehe ya kutumwa kwa jeshi hilo haijawekwa, ingawa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken hivi majuzi alisema ujumbe wa usalama nchini Haiti unaweza kutumwa "baada ya miezi kadhaa."

Tarehe 1 Januari 2024

Wakati huo huo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Kenya, Alfred Mutua, aliambia vyombo vy ahabari kwamba kikosi hicho kinapaswa kuwa tayari nchini Haiti ifikapo Januari 1, 2024, "kama si kabla ya hapo."

Haikubainika wazi mara moja ukubwa wa kikosi hicho. Awali serikali ya Kenya ilipendekeza kutuma maafisa 1,000 wa polisi. Kwa kuongeza, Jamaica, Bahamas na Antigua na Barbuda pia wameahidi kutuma wafanyakazi.

Mwezi uliopita, utawala wa Rais wa Marekani Joe Biden uliahidi kutoa vifaa na dola milioni 100 kusaidia jeshi hilo.

Uingiliaji kati wa kimataifa nchini Haiti una historia ngumu. Ujumbe wa kuleta utulivu ulioidhinishwa na Umoja wa Mataifa nchini Haiti ambao ulianza Juni 2004 ulikumbwa na kashfa ya unyanyasaji wa kijinsia na kuanzishwa kwa kipindupindu. Misheni hiyo ilikamilika Oktoba 2017.

Wakosoaji wa ujumbe ulioidhinishwa wa Jumatatu unaoongozwa na Kenya pia wamebainisha kuwa polisi katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki kwa muda mrefu wamekuwa wakishutumiwa kwa kutumia mateso, nguvu kupita kiasi na unyanyasaji mwingine.

TRT Afrika