Umoja wa Mataifa umeeleza kusikitishwa kwake na kuzorota kwa hali ya kibinadamu katika mikoa mitatu ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambapo karibu watu milioni 3.3 wameyakimbia makazi yao tangu Machi 2022.
Wanamgambo na makundi ya waasi yamevamia sehemu kubwa ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa miongo kadhaa, na kuchangia vita ambavyo vilipamba moto katika miaka ya 1990 na 2000.
Kundi moja mahususi lenye silaha, M23, limeteka maeneo mengi ya eneo la Kivu Kaskazini tangu 2021 baada ya kuanza mashambulizi tena.
Umoja wa Mataifa ulionya siku ya Alhamisi kwamba ili kukidhi mahitaji ya watu walioathiriwa na ghasia katika eneo hilo, wafanyakazi wa kibinadamu wanahitaji ufadhili wa zaidi ya dola bilioni 1.5.
"Hali ya kibinadamu huko Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, ambayo tayari ni changamoto , imezorota katika miezi ya hivi karibuni, na imekuwa muhimu kuongeza kiwango cha operesheni yetu," Suzanna Tkalec, mratibu wa Umoja wa Mataifa wa misaada ya kibinadamu ya muda nchini DRC, alisema.
Msaada kwa kwa watu 910,000
Mashirika ya kibinadamu yamesambaza misaada na usaidizi kwa zaidi ya watu 910,000 katika majimbo hayo matatu katika muda wa wiki sita zilizopita, ofisi ya Umoja wa Mataifa ilisema.
Lakini ifikapo mwisho wa mwaka, Umoja wa Mataifa, Shirika la Msalaba Mwekundu na mashirika yasiyo ya serikali zitahitaji kutoa msaada wa dharura kwa karibu watu milioni 5.5, UN ilisema.
Serikali ya DRC na mataifa kadhaa ya Magharibi ikiwa ni pamoja na Marekani na Ufaransa wanaishutumu Rwanda kwa kuunga mkono kikamilifu kikundi cha M23, Lakini Kigali inakanusha.