Shirika la Umoja wa mataifa la Chakula duniani, yaani World Food Programme linasema maghala yake, ofisi na nyumba za wageni katika maeneo kadhaa zimeporwa kabisa.
WFP inasema maghala mengine yamechomwa na mengine kuharibiwa.
"Wizi mkubwa unaoendelea hivi sasa nchini Sudan haukubaliki," Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa WFP Cindy McCain amesema," karibu 25% ya chakula cha WFP kimeibiwa ofisi zetu zinaporwa.”
“Ukosefu wa usalama sasa unafanya kazi kuwa karibu kutowezekana, hasa katika maeneo yenye migogoro kama vile mji mkuu Khartoum na katika eneo la Darfur," Mkurugenzi wa WFP Sudan Eddie Rowe ameeleza.
"Zaidi ya tani 17,000 za chakula zinazopelekwa kwa watu walio na njaa zaidi nchini humo zimeporwa kutoka kwenye maghala na malori yetu," Mkurugenzi wa WFP Rowe amesema.
Katika taarifa yake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gutteres ameutaja uporaji huo kuwa ni ‘ukiukaji wa vituo vya kibinadamu.
Kabla ya mzozo WFP ilipanga kusaidia zaidi ya watu milioni 7 nchini Sudan, mzozo huo hata hivyo utaongeza idadi hii.
Tayari, WFP Sudan ilikabiliwa na upungufu wa dola za kimarekani milioni 300 katika kipindi cha miezi sita ijayo - hata kabla ya idadi ya njaa inayoongezeka leo.
Vita nchini Sudan kati ya jeshi la Sudan na vikosi vya Rapid Support Forces vilianza tarehe 15 mwezi Aprili mwaka huu.
Wananchi wengi wamelazimika kukimbia makwao katika maeneo yaliyoathirika zaidi na vita. Wengine wamelazimika kuwa wakimbizi katika nchi jirani za Chad, Misri , Sudan Kusini na Ethiopia.
Huku ikiongeza juhudi za operesheni yake zaidi, Shirika la WFP linasema linalenga kutoa msaada kwa takribani watu milioni tano nchini Sudan wenye mahitaji ya dharura.