Na Coletta Wanjohi
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Serikali ya Sudan Kusini inasema iko tayari kwa uchaguzi mkuu, wa kwanza tangu nchi hiyo ipate uhuru wake mwaka 2011 kutoka kwa Sudan.
"Watu wa Sudan Kusini wanataka uchaguzi na tutakuwa na uchaguzi Disemba 2024," James Morgan, Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan Kusini aliiambia TRT Afrika.
Tangu uhuru, nchi hiyo imekuwa chini ya urais wa Salva Kiir.
Wakati serikali ya Sudan Kusini ikionyesha azma ya kufanya uchaguzi huo mwishoni mwa mwaka, kwa upade wake, Umoja wa Mataifa umeonyesha wasiwasi kwamba taifa hilo changa barani Afrika bado halijakuwa na nyenzo za kuandaa uchaguzi utakao kuwa huru na wa haki.
"Kwa hali ilivyo sasa, Sudan Kusini haiko tayari kwa uchaguzi na mengi yanahitajika kufanywa," Jean-Pierre Lacroix Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Operesheni za Amani ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
"Uchumi mchanga umezidisha mapigano juu ya rasilimali na kusababisha ukosefu mkubwa wa ajira unaoathiri vijana," aliongeza.
Umoja wa Mataifa unataja changamoto kama "ushindani wa kisiasa kati ya wasomi wanaotawala, kuongezeka kwa mapigano kati ya jamii na mkazo unaosababishwa na wimbi la wale wanaotoroka vita katika nchi jirani ya Sudan."
Kuahirishwa kwa uchaguzi
Baada ya uhuru kutoka kwa Sudan tarehe 9 Julai 2011, taifa hilo lilipanga kufanya uchaguzi Julai 2015, lakini mpango huu ulikatizwa na mzozo wa ndani uliozuka Disemba 2013.
Mgogoro wa kuwania madaraka kati ya serikali ya rais Salva Kiir na makamu wake wa wakati huo Riek Machar ulizusha vita ambavyo vililemaza mipango mingi ambayo nchi hiyo ilikuwa nayo ilipoadhimisha uhuru wake.
Mzozo huo ulisababisha mzozo wa kibinadamu ambao uliripotiwa kupoteza maisha ya watu 400,000 na zaidi ya watu milioni 5 kukimbia makazi.
Takriban nusu ya hawa walikimbilia nchi jirani za Sudan, Ethiopia na Uganda na wengine walikuwa wakimbizi wa ndani.
"Tunasema kwamba watu wanajifunza kutoka zamani, historia yenyewe ni mwalimu kwa hivyo watu wengi nchini Sudan Kusini wamejifunza kuwa vita havikuwa vya thamani yoyote," Morgan anaiambia TRT Afrika.
Bunge la Sudan Kusini lilipiga kura mwezi Aprili 2015 kurekebisha katiba ya mpito ya 2011 ili kuongeza muda wa urais na ubunge hadi tarehe 9 Julai 2018.
Mwaka huo huo, baada ya miaka ya kufanya maongezi ya amani, serikali ya Rais Salva Kiir, kikundi kinachoongozwa na aliyekuwa akimpinga Riek Machar na vikundi vyengine vilifanya makubaliano ya amani ambayo yalimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Na hapo kipindi cha uongozi cha mpito kikaamualiwa kuwa kitakuwa miaka mitatu na uchaguzi kupangwa tena mwaka wa 2023.
Lakini mnamo 2022, serikali ya mpito na upinzani walikubaliana kuisogeza mbele tarehe ya uchaguzi hadi mwishoni mwa 2024.
Safari ya kutafuta amani na utulivu
Baada ya miaka mingi ya mapigano na majaribio kadhaa ya kusitisha mapigano, serikali ya Sudan Kusini, vyama vya siasa vya upinzani vilitia saini Mkataba Uliohuishwa wa Utatuzi wa Mzozo katika Jamhuri ya Sudan Kusini (R-ARCSS), tarehe 12 Septemba 2018 huko Addis Ababa, Ethiopia.
Hii ilitoa fursa ya kuundwa kwa Serikali ya Mpito iliyohuishwa ya Umoja wa Kitaifa (RTGoNU), ambayo ilieleza muda wa kufanyika kwa uchaguzi ili kuihamisha nchi kutoka serikali ya mpito.
Walakini, utekelezaji wa masuala yaliyowekwa ulicheleweshwa na ambayo pia iliathiri uchaguzi ambao ulisukumwa hapo awali hadi 2023.
Mnamo Agosti 2022, sheria ya mpito iliongeza muda wake, kutoka miaka miwili hadi Februari 2025. Na ilipanga uchaguzi wa Disemba 2024.
"Makubaliano ya amani yaliyoimarishwa yalikuwa yakiendelea vizuri tu lakini kuchelewa kwa kutimiza mambo kadhaa ulisababishwa na mlipuko wa UVIKO 19 na mambo mengine," Waziri Morgan anaielezea TRT Afrika.
"Ndio maana viongozi waliamua kufanya kilichoitwa "ramani ya utimizaji," ambayo ilikuwa ni miezi 24 ya ziada ili kukamilisha kile ambacho hakijakamilika kwa uongozi wa mpito ambao uliidhinishwa na makubaliano ya 2018," Morgan anaongeza.
Kulingana na Umoja wa Mataifa "mfumo mpya wa kudumu wa kikatiba, maelezo ya usajili wa wapiga kura, mpango wa usalama wa uchaguzi, vikosi vya usalama vilivyofunzwa vyema, vilivyo na vifaa na vilivyounganishwa, na utaratibu wa kutatua mizozo ya uchaguzi" ni vikwazo vikubwa kwa uchaguzi huru na wa haki Sudan Kusini."
Serikali ya Sudan Kusini inasema baadhi ya masuala yatatatuliwa kwa wakati. "Hakuna wakati ambao tutakuwa tayari kabisa kwa uchaguzi, baadhi ya watu daima watasema tusubiri. Chaguzi hizi ni za wananchi, watu wa Sudan Kusini wanataka uchaguzi na watakuwa nao,” Morgan anaiambia TRT Afrika.
Uchaguzi mkuu wa Sudan Kusini utakuwa mojawapo ya chaguzi 15 barani ambazo Umoja wa Afrika umepanga kufanya uangalizi mwaka 2024 . Inasema hii ni "njia ya demokrasia ya kweli."
Baadhi ya wataalamu wanasema kufanyika kwa uchaguzi nchini humo kunaweza kuwa kichocheo kinachohitajika zaidi kwa miundo ya utawala bora na mageuzi ambayo yatainua maisha ya zaidi ya watu milioni 11 wa Sudan Kusini ambao tangu uhuru bado hawajafurahia utulivu na amani kamili.
Kufikia sasa rais aliyeko madarakani Salva Kiir ndiye pekee ambaye ameelezea nia yake ya kuwania kiti cha juu katika uchaguzi wa Desemba 2024.