Vita nchini Sudan vinaendelea tangu Aprili mwaka huu / Picha: AP Archive

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limeonya kwamba huku dunia ikizingatia sasa mzozo wa Gaza, idadi ya watu wanaokimbia makazi yao nchini Sudan imeanza kuongezeka tena huku vikosi vya RSF vikielekea Nyala, mji wa pili katikati mwa nchi hiyo, Darfur.

Vita kati ya wanajeshi watiifu kwa Mkuu wa Jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhane na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) cha Jenerali Mohamed Hamdane Dagalo vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 9,000 tangu Aprili, hii ni kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa.

"Miezi sita na watu milioni sita wanalazimishwa kuhama, hiyo ni wastani wa milioni moja kwa mwezi; ni mateso ya kutisha," Mamadou Dian Balde, afisa wa juu wa kanda wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR).

" Takriban watu milioni sita ambao wamekimbia, milioni 1.2 wameondoka nchini, "Watu wanajikuta wakiomba omba, na maisha yao yametatizika kabisa," afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema.

Matukio ya kuhuzunisha

Afisa mwingine wa Umoja wa Mataifa katika eneo hilo, Dominique Hyde, aliandika kwenye mtandao wa kijamii siku ya Alhamisi kwamba alishuhudia "matukio makubwa" katika mipaka ya Sudan.

Mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhane na mkuu wa Rapid support Forces  Jenerali Mohamed Hamdane Dagalo hawajakubaliana kusitisha vita / picha : Others 

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alisema "anafadhaishwa sana" na taarifa kuhusu "mashambulizi makubwa yanayokaribia" ya vikosi vya kijeshi vya Sudan huko El-Facher, mji mkuu wa Darfur Kaskazini.

Shirika la Umoja wa Mataifa linaonya kwamba watu wengi zaidi kutoka Darfur wanasukumwa kusini, kwanza hadi Chad katika wiki za hivi karibuni na sasa Sudan Kusini.

Mamadou Dian Balde alisema kipaumbele ni kusitisha mapigano, akibainisha kuwa mazungumzo yanayoendelea katika Jeddah ya Saudi Arabia yanahitaji "kufanikiwa kusimamisha mapigano."

Mazungumzo ya haraka

Mazungumzo kati ya pande zinazozozana yalianza tena mwishoni mwa Oktoba. Majaribio ya awali ya upatanishi yalisababisha tu mapatano mafupi, ambayo yalikiukwa kimfumo.

Wakati huo huo, "lazima tupunguze mateso (ya wakimbizi) kwa kutoa rasilimali kwa watu hawa ambao idadi yao inaongezeka tu," Balde alisema.

"Mpango huo umepokea tu asilimia 38 ya ufadhili unaohitajika, wakati mahitaji yanaongezeka," alisema afisa huyo wa Umoja wa Mataifa, akibainisha kuwa wakimbizi wengi walikuwa wakienda maeneo yenye hali duni zaidi ya Sudan Kusini na kusini mwa Chad, ambako wenyeji haziwezi kuwapokea."

Vita hivyo vimepeleka zaidi ya watu kukimbilia nchi jirani za Chad, Sudan Kusini , Misri na Ethiopia / Picha Reuters 

Kambi za wakimbizi

Umoja wa Mataifa unasema mmiminiko mkubwa wa wakimbizi unamaanisha kuna haja ya kujenga kambi mpya.

"Ni jambo la mwisho tunalotaka kufanya," afisa huyo wa Umoja wa Mataifa alisema, lakini "Tunahitaji kuunda kambi mpya kwa sababu idadi ya watu iko mpakani na katika hali mbaya sana."

Pia alitoa wito wa kusaidia jamii za wenyeji. "Tunataka maendeleo. Tunapaswa kuwekeza katika maeneo haya kwa sababu ikiwa tu tunatoa msaada kwa wakimbizi, itazua mvutano, na mivutano inaweza kusababisha vurugu."