Na Coletta Wanjohi
Addis Ababa, Ethiopia
Marais na viongozi wa serikali barani Afrika wameanza mkutano wao wa kila mwaka hapa katika makao makuu ya Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa nchini Ethiopia.
Watakutana tarehe 15 na 16 Februari 2024, kujadili masuala muhimu ya bara hili.
Mwaka huu 2025, bara hili limejiwekea mada ambayo itazingatia "Haki kwa Waafrika na watu wa asili ya Kiafrika kulipwa fidia"
Makoloni ya zamani kama vile Ureno, Uingereza, Ufaransa, Ubelgiji, Uholanzi, na Ujerumani wanawajibika pakubwa katika suala la biashara ya utumwa na ukoloni.
Umoja wa Afrika unataka haki ipatikane kwa Waafrika walioko barani na nje ya bara, ikitambua madhara makubwa yaliyosababishwa na biashara ya utumwa Atlantiki, ambapo pia kulihusisha utumwa, ukoloni na ukoloni mamboleo.
Lakini ni kwa kiasi gani AU itafanikiwa kuyawajibisha mataifa ya kikoloni kwa hali iliomalizika miongo mingi iliyopita?
Baadhi ya nchi tayari zinadai haki kutoka kwa mamlaka hizo za kikoloni.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC inataka kulipwa fidia kutoka kwa Ubelgiji kwani nchi hiyo imekiri kutekeleza ubaguzi wa rangi na vitendo vya unyanyasaji nchini humo.
Jamii za Namibia ambazo mababu zao waliuawa na vikosi vya wakoloni wa Ujerumani na mali zao kuchukuliwa zaidi ya karne moja iliyopita wanataka Ujerumani iwajibike kwa mateso hayo.
Ufaransa iliotawala zaidi ya nchi 20 magharibi na kaskazini mwa Afrika sasa hivi inapoteza ushawishi wake kwa mataifa hayo.
Nchi kama Ivory Coast, Chad, Senegal, Mali, Niger na Burkina Faso zimeiomba Ufaransa kuondoa wanajeshi wake katika maeneo yao.
Nchini Kenya bado kuna ishara za makovu ya ukandamizaji wa Waingereza wakati wa kupigania uhuru.
AU inasema mamlaka za kikoloni ambazo zilichukua mali ya Waafrika bado zinaweza kulipa kwa njia tofauti.
Inasema kuendelea kutambua na kuweka kumbukumbu za athari za ukoloni na utumwa kwa jamii za Kiafrika ni muhimu kwa ushahidi wa matukio hayo.
Malipo ya fidia kwa mataifa ya Kiafrika na jamii zilizoathiriwa na unyonyaji wa wakoloni yanaweza kuwa kwa njia ya uwekezaji kutoka kwa mataifa yalokuwa makoloni, hasa katika maeneo ya miundombinu, elimu, na huduma za afya ili kusaidia kuimarisha uchumi wa mataifa hayo.
Afrika inataka ardhi irejeshwe au jamii zilipwe fidia kwa maeneo yaliyonyakuliwa. Bara linadai kwamba urithi wa Kiafrika uliopotea urejeshwe kupitia kwa mfano ufadhili wa taasisi za kitamaduni, miradi ya elimu, na kurejeshwa kwa vito vya kitamaduni.
Haya yote AU inasema yanaweza kufanywa kwa kuwepo kwa shinikizo la kidiplomasia au hata hatua za kisheria katika ngazi ya kimataifa. Na kwa mikakati hii, Bara la Afrika linatazamia kuwapa watu wake haki katika mwaka huu wa 2025.