Kikundi cha M23 kimeingia mji wa Bukavu, Mashariki mwa DRC / Picha: AP

Mkutano wa Umoja wa Afrika uliokamilika nchini Ethiopia umejadili kwa kina suala la usalama wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Marais na viongozi wa serikali walikutana 15 na 16 Februari jijini Addis Ababa , kwa mkutano wao wa kila mwaka.

Marais na viongozi wa Afrika wameunga mkono maazimio yaliyotolewa katika mkutano wa viongozi wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika uliofanyika nchini Tanzania Februari 8, 2025.

Mkutano huo umetaka kikundi cha M23 kusitisha mashambulizi mara moja na kusisitiza umuhimu wa mazungumzo ya amani.

"Sote tuna wasiwasi sana kuhusu vita vya kikanda mashariki mwa DRC. Tulisisitiza haja ya kuwepo na tahadhari na M23 pamoja na wafuasi wake kupokonywa silaha na kuondoka kwenye uwanja wa ndege wa Goma na maeneo mengine yanayokaliwa, " Bankole Adeoye, Kamishna wa Umoja wa Afrika wa amani na masuala ya siasa alisema.

Mkutano wa Umoja wa Afrika umeitaka M23 pamoja na wafuasi wao kujiondoa mara moja maeneo ya Mashariki mwa DRC. Viongozi hao wamesisitiza umuhimu wa kuheshimu uhuru wa kisiasa na maeneo ya DRC.

" Mashambulizi haya mapya hayatakiwa kuwa mzozo ambao utavuruga shughuli za watu na mfumo wa kijamii ambao tayari umedhoofika sana katika kanda. Njia pekee ya kutatua tatizo mashariki mwa DRC ni kwa pande zote kujadiliana, " Bankole aliongezea.

Umoja wa Afrika unaitaka M23 kuheshimu makubaliano ya amani ambayo yalisainiwa na serikali ya DRC mwaka 2013, ambapo waliapa kuacha uasi.Imesema ni muhimu kwa wadau wote wa mgogoro huo kukubali mchakato wa amani wa Umoja wa Afrika unaosisitiza mazungumzo.

Mchakato huo wa AU unaongozwa na Rais wa Angola João Lourenço.Wakati huo huo, Rwanda inaendelea na msimamo wake wa kukana kuiunga mkono M23 licha ya wao kuendelea kushutumiwa.

Umoja wa Afrika vilevile unasisitiza kuwa M23 sharti ikubali kusalimisha silaha na kujumuishwa tena katika jeshi la taifa la DRC.

Viongozi wa Afrika pia wamesema kuwa uchimbaji usio halali wa madini nchini DRC unaongeza kutokuwepo kwa usalama, na kuvitaka vikundi vingine vyenye silaha kama mamluki na mashirika binafsi ya huduma ya ulinzi yaondoke DRC.

Hata hivyo, licha ya maamuzi haya na jitihada za kuzuia machafuko, kikundi cha M23 bado kinaripotiwa kuendela kufanya mashambulizi katika maeneo ya DRC.

TRT Afrika