Makao Makuu ya Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia/ Picha : Reuters

Na Mohamed Guleid

Licha ya fursa lukuki zinazopatikana ndani yake, bara la Afrika bado linakabiliana na changamoto nyingi, zikiwemo umaskini, magonjwa na migogoro ya kisiasa.

Bara hili bado limesalia kwenye minyororo ya migawanyiko ya kihistoria na mapambano ya kujitegemea.

Hata hivyo, mwangwi mkubwa wa mabadiliko unaendelea kuvuma, ukisisitiza uandikwaji upya kwa simulizi za Afrika. Ni wakati muafaka kuimarisha taasisi zetu, ili ziweze kuenenda na matakwa ya kimataifa.

Hali kadhalika, sauti za uchechemuzi wa umoja na ushirikiano barani Afrika sio za kupuuzwa.

Kwa upande wake, Umoja wa Afrika(AU) una nafasi kubwa na ya kipekee katika kuchagiza dhana hii. Hata hivyo, umoja huu bado unakabiliwa na changamoto katika kufikia muafaka baina ya nchi wanachama wake kutokana na sababu mbalimbali.

Kwa kuanzia, urithi wa kihistoria wa ukoloni na mipaka ya 'kufikirika' imeliachia bara hilo mpasuko mkubwa, na kusababisha kutofautiana kwa maslahi ya kitaifa, tofauti za kitamaduni, na itikadi za kisiasa. Migawanyiko hii inafifisha maelewano katika masuala muhimu ya kijamii.

Mbali na hayo, tofauti za kiuchumi na na viwango tofauti vya maendeleo kati ya nchi wanachama zimeibua vipaumbele tofauti.

Sera za kikoloni zimeliacha bara la Afrika katika mgawanyo mkubwa wa kiuchumi./Picha:Getty

Mgawanyiko kiuchumi

Masuala ya kisiasa na mienendo ya kikanda ni kati ya sababu za migawanyiko hii, kwa maana kwamba baadhi ya mataifa hutafuta nguvu za ushawihshi na utawala, na hivyo kuchochea ushindani badala ya ushirikiano.

Migongano ya kimaslahi mara nyingi hutokea, hasa kuhusu mizozo ya maeneo, ugawaji wa rasilimali, au itikadi za kisiasa, zinazozuia kufanya maamuzi ya pamoja.

Mbali na hayo, michakato ya AU katika kufanya maamuzi ni mirefu na yenye kuchosha na hivyo kuzorotesha hatua na makubaliano kwa wakati unaofaa kuhusu masuala muhimu huku nchi wanachama zikijitahidi kulinda maslahi yao binafsi.

Vivyo hivyo, ushawishi kutoka nchi za nje, ikiwa ni pamoja na kuingiliwa na mamlaka za kimataifa unaweza kufanya mambo kuwa magumu zaidi, hasa katika kushawishi maamuzi ndani ya umoja huo.

Hata ukizingatia masuala ya kihistoria, kiuchumi na ushawishi kutoka nje, bado AU inakumbana na changamoto kwenye kutafuta maelewano na kusaka ya mambo muhimu kwa bara hili.

Juhudi za kukuza umoja zinahitaji kupitia changamoto kadha wa kadha, ili kuunda muungano wenye nguvu na mshikamano kwa ajili ya maendeleo ya pamoja ya Afrika.

Hivi karibuni, Chuo Kikuu cha cha Lukenya cha nchini Kenya kilianzisha taasisi ya ushirikiano wa Afrika, kiashiria muhimu cha kufikia hatua hiyo inayosubiriwa kwa hamu.

Taasisi hiyo inalenga kuelimisha, kufanya tafiti bunifu na kukuza umoja kama mwanga wa umoja kati ya mataifa ya Afrika.

Ushirikiano kati ya mataifa ya Afrika, hasa katika ukanda wa kusini, bado ni wa kusuasua.

Muunganiko wa anga ndani ya bara hili unasalia kuwa na dosari za kushtua na hivyo kudumaza biashara ya ndani, ikiwa ni asilimia 14 tu.

Ukweli huu ni msisitizo bayana kuwa Afrika ina uwezo mkubwa kiuchumi ambao bado haujatumika.

Mkutano wa Umoja wa Afrika uliofanyika Februari, 2022./Picha : Reuters

Afrika moja

Mtazamo wa Profesa Patrick Loch Otieno Lumumba wa Afrika ni kuwa na bara lisilo na mipaka, dhana inayohuisha ushirikiano dhabiti wa Kiafrika, bila kujali tofauti za rasilimali au uchumi, bali fahari ya bara lenyewe.

Hata hivyo, kufikia malengo ya aina hii si kazi rahisi kwani Afrika imebakiwa na majeraha makubwa yaliyosababishwa na ukoloni.

Vile vile, dhana hii bado inapambana na mzigo mzito wa kuponya majeraha haya ya kihistoria kupitia kukuza biashara ya ndani na ushirikiano wa wananchi wa Afrika.

Harakati za namna hii zinalenga kuondoa vizuizi vinavyozuia biashara na uhamaji ndani ya bara letu.

Ni muhimu kukuza ushirikiano na kuondoa vikwazo vinavyozuia biashara ya ndani ya Afrika. Vivyo hivyo, taasisi ya Chuo Kikuu cha Lukenya ina jukumu la kupanga mikakati ya kukuza mwingiliano wa kibiashara kati ya nchi za Kiafrika.

Hata hivyo, ni lazima tukubiliane na ukweli kwamba aafanikio yetu hadi sasa yamepungua sana kuliko uwezo wetu.

Hata mkataba wa Eneo Huru la Biashara barani Afrika (AfCFTA), ulioridhiwa na nchi kadhaa za Afrika umeweka bayana azma ya kuongeza kazi ya kufanya biashara ya ndani.

Juhudi za taasisi iliyo chini ya Chuo Kikuu cha Lukenya inapaswa kuvuka nyanja za taaluma, na hivyo kuchochea ushirikiano unaoonekana unaounganisha mipaka na lugha.

Hata tamaduni, ushirikiano wa kielimu, na juhudi za pamoja za utafiti ni muhimu katika kuunda utambulisho wa pamoja kati ya mataifa ya Afrika.

Mbali na hayo, ni muhimu kutegemea uimarishaji wa miundombinu, hasa katika usafiri na mawasiliano, kama nguzo ya biashara ya ndani ya Afrika.

Miunganisho iliyoboreshwa ya anga, barabara na bahari haitarahisisha tu ufanywaji wa biashara barani Afrika, bali itakuza mabadilishano ya kitamaduni na kustawisha mwingiliano kati ya watu.

Uboreshaji miundombinu utarahisisha biashara na pia kukuza tamaduni barani Afrika./Picha: Reuters

Taasisi hiyo, pia inapaswa kutumika kama jukwaa la midahalo inayoshughulikia masuala ya msingi yanayozuia umoja wa Afrika. Majadiliano yanayohusu utawala, maendeleo endelevu, na ushirikiano wa kijamii na kisiasa lazima yaongoze safari yetu ya pamoja kuelekea Afrika iliyounganishwa na yenye ustawi.

Hata hivyo, ili hili lifanikiwe, juhudi madhubuti kutoka mataifa yote ya Afrika zinahitajika.

Ni wakati muafaka kuachana na mipasuko ya kihistoria, kukumbatia urithi wetu wa pamoja, na kupiga hatua kuelekea Afrika inayostawi - bara ambalo linasimama kidete kama mwanga wa matumaini, maendeleo, na uthabiti usioyumba.

Mwandishi wa makala hii ni mratibu wa Kitaifa wa miradi ya NEDI.

TRT Afrika