Na Yusuph Dayo
Nguvu za nje kama vile mzozo wa Urusi na Ukraine, Covid 19 na mabadiliko ya hali ya hewa yamesababisha matatizo makubwa katika uchumi wa dunia na hii inajitokeza wazi Afrika.
Hii ilifichua hatari ya msingi ya utegemezi wa madeni ambayo ilizipa wito wa kuamka nchi za Kiafrika kujitegemea zaidi wanapo tayarisha bajeti zao kwa mwaka wa fedha wa 2023-24.
Lakini wachambuzi wanasema wadeni wa kigeni walichukua jukumu kubwa zaidi kwani waliwabana walipa kodi kukusanya sehemu kubwa ya hazina ya umma katika ulipaji wa mkopo na viwango vya juu vya riba.
Mwanauchumi wa Tanzania Beatrice Kimaro anasema kukata mikopo kutoka nje kutanufaisha wananchi kwa muda mrefu.
‘’Kuna jitihada kubwa ukilinganisha na mwaka jana, kwamba serikali hizi kwa makusudi zinatafuta vyanzo vya fedha zao ndani ya nchi. Wanatanguliza kukusanya kodi,’’ anasema.
Uvumilivu una manufaa
‘’Ukiangalia Kenya kwa mfano wanaongeza kodi ya VAT hadi karibu 16%. Watahisi kubanwa kidogo kwa muda, lakini nadhani ikiwa kodi zitasambazwa vizuri, nchi itakuwa bora zaidi kuliko kuongezeka kwa mikopo ya nje.’’
Kumekuwa na msukumo kutoka kwa wakenya ambao wanapinga ongezeko hili la kodi, wakidai hali ya maisha tayari ni ngumu.
Beatrice anaonya kuwa serikali inahitaji kuwa na busara katika kuwatoza watu kodi ili kuhimiza uwekezaji zaidi.
‘’Kodi kubwa kwa wananchi itasababisha watu kuogopa kuwekeza nchini. Hiyo itamaanisha kushuka kwa pato la taifa. Lakini ushuru nchini Tanzania kwa mfano sio juu kama ilivyo pendekezwa nchini Kenya…. Sitashangaa kusikia baadhi ya wawekezaji kutoka Kenya wakihamia Tanzania kutafuta kodi nzuri.’’ Anaongeza.
Nchini Uganda, mbali na kuongeza ushuru wa ndani serikali imeweka kipaumbele kulipa madeni yaliyopo. Beatrice anasema hii inaonyesha uchovu katika kuhudumia madeni ya muda mrefu ambayo yanalemaza maendeleo.
‘’Kulipa madeni ya nje si kazi rahisi. Na kadri unavyozidi kuwa na deni kutoka nje ndivyo utakavyokuwa umefungwa katika malengo yako ya ukuaji. Unaona Uganda sasa imetenga karibu asilimia 30 ya bajeti yake ili kufidia hili, ambalo nadhani ni hatua nzuri.’’ Anasema Beatrice.
Wamepata somo gumu
Nchi za Afrika katika miaka ya hivi karibuni zimekuwa zikizungumza dhidi ya kutegemea madeni ya nje.
Hii ni kwa sababu madeni mengi yanakuja na masharti magumu wakati mwingine yanayotishia kuingilia namna nchi zinaendeleza shughuli zake.
Beatrice anasema inaonekana nchi nyingi zimejifunza somo japo kwa njia ngumu.
‘’Unapokuwa tegemezi kwa watu wa nje, basi tarajia kudhibitiwa. Nchi nyingi za kiafrika zimeonyesha kutoridhishwa na mwenendo huu na zinahimizana kuachana na hilo.’’ Anasema. ‘’Deni ni deni na huwa linakuja na riba na kadri riba inavyopanda ndivyo unavyozidi kuwaumiza wananchi ambao ndio wanaolipa’’.
Beatrice pia anasema ni bora kujitegemea katika nyakati hizi zisizotabirika.
‘‘Wakati bajeti yako inalingana na hazina yako ya ndani, basi hutatumia kupita kiasi. Lakini unapotegemea kutoka nje, utafanya nini ikitokea dharura kama vile janga la Covid 19 au mabadiliko ya hali ya hewa na wadeni wa kigeni kuamua kupunguza au kuelekeza matumizi yao kwingine?’’ anahoji.
Beatrice anasema inatia matumaini kuona hivi sasa Afrika Mashariki inaondokana na utegemezi huu wa nje polepole, lakini watahitaji kuwaelimisha watu wao zaidi kuhusu kodi ili serikali na wananchi waelewane na kufanya kazi bega kwa bega.
‘’Miradi yako mingi inapofadhiliwa na watu wa ndani, inakupa furaha. Watu watakuwa na fahari.’’ Anasema. ‘’Unajisikia vizuri kuona barabara katika nchi yako inafadhiliwa kikamilifu na wewe, raia. Au kliniki inafadhiliwa na kodi uliolipa. Utapata fahari kubwa.’’