Na Kevin Philips Momanyi
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Wabunge nchini Kenya na raia wa nchi hiyo ni kama wamepigwa na ‘kitu kizito kichwani’ kufuatia taarifa za hivi karibuni kuhusu kuhesabu kwa samaki.
Wizara ya Madini, Uchumi wa Bluu na Masuala ya Bahari ya nchi hiyo imeripotiwsa kutumia shilingi bilioni 1.6 ambayo ni sawa na zaidi ya Dola milioni 12.4 kuhesabu samaki walioko ndani ya Bahari ya Hindi kwa mwaka wa fedha wa 2023-2024.
Lakini je, Samaki huhesabiwa vipi na ni kwa sababu gani?
Ni vigumu kwa wataalamu au hata wanasayansi kujua idadi ya samaki wote walioko baharini. Kinachofanyika ni ukusanyaji wa takwimu isiyo halisi na kuja na taswira au ubashiri fulani wa kiwango cha Samaki.
Wataalamu hao hukusanya takwimu nyingi iwezekanavyo kwa kutumia njia tofauti ikiwemo wavuvi na vifaa maalumu vyenye kutumia mawimbi kuhesabu samaki. Unajua vyombo hivyo vinafanyaje kazi?
Hutoa mawimbi kutoka chini ya maji, ambayo hukutana na Samaki na baadaye hurudi kama mwangwi fulani wa sauti na kisha kunakiliwa.
Kwa kuchanganua inachukua muda gani kwa mwangwi huu kurudi na nguvu za mwangwi wenyewe, wanasayansi wanaweza kukadiria ukubwa wa Samaki na kina cha maji yenyewe.
Hivyo basi, kiasi kikubwa cha mwangwi huashiria idadi kubwa ya Samaki.
Kipimo cha namna hii hurudiwa mara kadhaa na huchukuliwa ili kukadiria jumla ya idadi ya samaki. Kupitia njia hii pia, wanasayansi huweza kung’amua mazalia ya samaki na idadi ya mayai yaliyotagwa, uwiano wa Samaki wa kiume na wa kike, kiwango cha ukuaji na hata mifumo ya uhamaji wa Samaki hao.
Mamlaka za nchi mbalimbali hutumia matokeo haya kudhibiti shughuli za uvuvi, kutenga maeneo maalumu ya kuvulia samaki, kuweka kanuni za shughuli za uvuvi na kutoa kiwango cha chini na cha juu zaidi cha samaki wanaoweza kuvuliwa.
Hata hivyo, wabunge nchini Kenya Kenya wameonesha wasiwasi wao kuhusu gharama zilizotumika katika zoezi hilo, wakisisitiza kuwa kwanini kiasi kikubwa kama hicho kitumike kwenye sekta inayoshindwa hata kutengeneza Shilingi milioni 50 kwa mwaka?
Kwa taarifa yako tu, hadi sasa Shilingi bilioni 3.6 za Kenya ambazo ni sawa na Dola Milioni 27, zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza zoezi la kuhesabu Samaki ambalo litafanywa kwa awamu tatu.