Mbali na kuwa mnyama mkubwa zaidi nchi kavu, Tembo ana vitu vingi vinavyovutia./ Picha: Getty Images

Na Edward Qorro

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Mauaji ya tembo, mnyama mkubwa zaidi aishiye nchi kavu yamepungua kutoka matukio 8 hadi kufikia 3, kwa mwaka 2023.

Kwa mujibu wa wasilisho la hivi karibuni kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), upungufu wa mauaji hayo unatokana na ulinzi kuimarishwa kwenye maeneo yaliyohifadhiwa ya nchi hiyo, pamoja na ushirikishwaji wa jamii katika mambo ya uhifadhi.

TAWA imehusisha upungufu wa mauaji hayo na mizoga michache iliyogundulika katika maeneo yaliyohifadhiwa nchini Tanzania.

"Kupitia operesheni zetu maalumu, tumeweza kutia hatiani washukiwa wa mauaji ya tembo," inasomeka sehemu ya wasilisho hilo.

Kulingana na wasilisho kutoka TAWA, jumla ya washukiwa wa ujangili dhidi ya Tembo 3,700 walikamatwa mwaka 2023, ukilinganisha na 4,800 waliotiwa nguvuni kwa mwaka 2016.

Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) inasema kuwa mauaji ya mnyama huyo yamepungua kutoka 18 kwa mwaka 2016 hadi kufikia 3 kwa mwaka 2023./Picha: TRT Afrika

Kwa mujibu wa Waziri ya Maliasili na Utalii nchini Tanzania, idadi ya tembo imeendelea kuongezeka kutokana na udhibiti na kupungua kwa matendo ya ujangili.

Mwaka 2019, nchi hiyo ilimtia hatiani Yang Feng Glan, mfanyabiashara kutoka China kwa makosa ya usafirishaji wa meno ya tembo 860 kati ya mwaka 2000 na 2014.

"Mnamo Aprili 12, 2022 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, alikamatwa mtuhumiwa mmoja raia wa China akiwa na bangili moja na kidani ambazo zilitambuliwa kuwa zimetengenezwa kwa meno ya tembo. Mtuhumiwa aliingia nchini Aprili 10 na siku mbili baadaye, alikuwa anaondoka kuelekea Bankok, Tailand," kwa mujibu wa wasilisho hilo.

Wimbi la ujangili na usafirishaji haramu wa meno ya tembo ulishika kasi barani Afrika, na kusababisha kupungua kwa tembo wa Afrika, wakati ujangili unaelezwa kuchangia upungufu wa zaidi ya nusu ya idadi ya tembo nchini Tanzania, kati ya 2009 na 2014.

TRT Afrika