Ujamaa kwa njia moja uliwasaidia Watanzania kuwa na umoja na kuimarisha usalama na amani./ Picha : Reuters 

Na Dayo Yussuf

Watalii wa Kiafrika hasa kutoka nchi jirani ya Tanzania wanashangazwa kila leo wanapofika nchini humo. Katika mpaka wowote ule, utapokewa kwa tabasamu, ukarimu na matamshi laini yanayokupa taswira ya amani na utulivu.

Iwapo umekuja Tanzania kuepuka zahma za miji yenye zahma kama Nairobi au Kampala au hata Lagos, basi umepatia hasa.

Na ndiyo iliyokuwa ndoto ya mwanzilishi wa taifa la Tanzania Mwalimu Julius Nyerere. Punde baada ya kutangazwa kwa uhuru, Mwalimu Nyerere alipendelea kurejesha ule Ubuntu, yaani undugu wa Kiafrika ulioonekana kuvurugwa na wakoloni.

Ndoto ya Mwalimu Nyerere ilikuwa kuwaunganisha Watanzania, washikane mkono hatua kwa hatua kuinuana na kujenga taifa lao pamoja. Na njia bora zaidi wakati huo, angalau kwa mtazamo wake ilikuwa kutekeleza sera ya Ujamaa au Socialism.

Lakini kwanini wazo zuri kama hili limegeuka kuwa karaha kwa Tanzania?

Utegemezi

Baadhi ya wataalamu wanaulaumu mfumo huu wa uongozi kwa kudidimiza hulka ya ushindani miongoni mwa raia na kupotea kule kujituma.

Tanzania ni nchi kubwa, yenye utajiri wa hali ya juu, unaojumuisha mali ya ardhini, kama madini ya kila aina, ikiwemo madini ya kipekee kama Tanzanite inayojivunia./ Picha : Reuters 

‘’Unajua ukitazama Ubepari, ni kule kujituma. Kadri unavyofanya kazi ndivyo unavyopata. Na unachopata ni chako. Kwa hiyo watu wanapata motisha kwa sababu ya tuzo yake,’’ anasema Agnes Kinyua, mhadhiri wa historia katika chuo kikuu cha Daystar jijini Nairobi. ''Kwa upande wake Ujamaa inamaana kufanya kazi kwa pamoja na kushirikishana katika tabu na raha. Tatizo ni kuwa unaleta uvivu. Wakati mwengine mtu anaona hata asipofanya kazi hatakosa riziki mdomoni.’’ Agnes anaambia TRT Afrika.

Tanzania ni nchi kubwa, yenye utajiri wa hali ya juu, unaojumuisha mali ya ardhini, kama madini ya kila aina, ikiwemo madini ya kipekee kama Tanzanite inayojivunia.

‘’Unajua Tanzania kihistoria ina kila kitu kwa manufaa yake. Kufikia wakati wa uhuru wa taifa, japo kuwa Capitalism haikuanzishwa toka mwanzo ndipo mambo yalianza kwenda mrama kwa taifa hilo,’’ anasema Agnes.

Lakini haya yote yanakuja na uwajibikaji wa ujasiriamali na uzalishaji mwanzo. Na iwapo wafanyakazi wenyewe hawana msukumo, basi mazao yanashuka.

‘’Watu walianza utegemezi kwa nchi, na wengi hawakupata ule msukumo wa biashara,’’ anaongeza Agnes.

Ujamaa kwa njia moja uliwasaidia Watanzania kuwa na umoja na kuimarisha usalama na amani. Wazungu wanasema 'Be your brothers Keeper' yaani ujali maslahi ya mwenzio.

Upweke wa sera katika kanda

Kingine ambacho kinalaumiwa kusababisha kushindikana kwa sera ya Ujamaa Tanzania ni kuwa ilikuwa nchi ya pekee katika kanda nzima iliyotekeleza sera hiyo.

Japo sera ya Ujamaa imedidimia kwa kiasi kikubwa, bado kuna athari zake zinajichomoza./ Picha: Reuters 

Majirani Kenya na Uganda, wanaoangaliwa na ndugu wa karibu wa Tanzania, walitimka na sera ya kujenga nchi kwa njia ya ushindani katika uwekezaji. Hii ilisababisha nchi hizi mbili, licha ya kupata uhuru wao kwa wakati mmoja, ziliweza kujisukuma zaidi kiuchumi na kuvutia uwekezaji kutoka nje kwa wingi, kwani ushindani wa kibiashara uliwapa fursa kila mtu kujaribu bahati yake.

Wengine wamefaulu na Ujamaa?

Wanahistoria wamelalamika kuwa sera ya Ujamaa haijaonekana kufaulu katika nchi yoyote.

‘’Ujamaa haujafanikiwa kokote duniani. Unajua ulianzia katika muungano wa Usovieti, USSR. Na nchi ambayo bado hadi sasa inatumia sera hiyo kikamilifu ni Korea ya Kaskazini. Lakini unaionaje, imekuwa gereza, na imegeuzwa kuwa mali inayomilikiwa na familia ya Kim Jong Un. Huwezi hata kusafiri nje ya nchi na hakuna anayejua kinachoendelea huko. Kwa hiyo ujamaa haujathibitika kufaulu kokote.’’ Agnes anaambia TRT Afrika.

Lakini kuna nchi ambayo imetafuta njia ya kuchanganya mifumo yao na Ujamaa, na kwa njia moja au nyingine wameweza kumudu japo kwa gharama.

‘’Nikikupa mfano wa Uchina, walikuwa na sera kamili ya Ujamaa hadi mwaka 1990,’’ anaelezea Agnes. ''Walikuwa na Ujamaa wa kijamii, Ujamaa wa kiuchumi na Ujamaa katika siasa. Lakini mwaka 1990 walibadilisha sera ya kiuchumi pekee kuwa ya Kibepari. Hii ndio ilisaidia kufungua uchumi wa Uchina, lakini kijamii na kisiasa bado wanadhibitiwa na sera za Ujamaa, ndio unaona wanawekewa vikwazo vya kupata watoto, au vikwazo vya kisiasa,’’ anasema Agnes.

Mbegu za Ujamaa

Tukirudi nchini Tanzania, japo sera ya Ujamaa imedidimia kwa kiasi kikubwa, bado kuna athari zake zinajichomoza.

‘’Kihistoria, mageuzi mengi huja kupitia mabadiliko ya vizazi. Mara nyingi vizazi vipya havijifungi na historia. Hawahisi kuwa wanawajibika kufuata mkondo wa vizazi vilivyowatangulia. Ukitazama Tanzania, hata mitaala yao ya shule imeanza kuwa ya utandawazi, wanajiunga na mifumo ya wengi duniani. Ni wazi kuwa ule msingi wa Ujamaa haujakwisha kabisa, lakini unaelekea kutokomea,’’ anaongeza Agnes.

Suala la iwapo Tanzania ilikuwa bora chini ya Ujamaa au la, ni sauala ambalo bado linajadiliwa vikaoni. Nadharia zimegawanyika huku wengine wakikumbuka kwa mapenzi namna mambo yalikuwa tulivu enzi zao ikilinganishwa na sasa.

Lakini wengine wanahoji kuwa baadhi wameshindwa kutenganisha Ujamaa na uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere, ambaye sifa zake zimetapakaa sio Tanzania tu bali hata bara zima na Ulimwenguni.

Kwa hiyo wanaona kukosoa sera aliyotumia ni sawa na kumkosoa Mwalimu mwenyewe.

TRT Afrika