Serikali ya Tanzania ina lengo la kuongeza idadi ya watalii wanaokuja nchini kufikia milioni tano ifikapo mwaka 2025./Picha: Getty

Na Edward Qorro

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Katika kudhibiti uhaba mkubwa wa dola unaoshuhudiwa katika mzunguko wa fedha nchini Tanzania, serikali imewataka wamiliki wa hoteli za kitalii zenye hadhi ya kati ya nyota 3 hadi 5, kuanzisha maduka ya kubadilishia fedha za kigeni ndani ya hoteli hizo.

Kupitia Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Emmanuel Tutuba, uamuzi huo pia unalenga kudhibiti maduka yasiyo rasmi ambayo yameendelea kushamiri wakati Tanzania ikiendelea kukabiliana na uhaba huo.

Katika kikao chake na wawekezaji katika sekta ya Maliasili na Utalii, kaskazini mwa Tanzania mwishoni mwa wiki, Tutuba ametoa mpaka Julai 1, 2024 kwa wamiliki wa hoteli hizo, kuanza kwa utekelezaji wa kanuni hiyo ambayo inalenga kurejesha mzunguko wa kawaida wa fedha za kigeni sokoni, hususani dola za Kimarekani.

Tutuba aliwahakikishia wamiliki wa hoteli hizo kuwepo kwa masharti nafuu wakati wa kuomba leseni za kuendesha maduka hayo ya kubadilishia fedha, huku akilalamikia mwitikio hafifu katika mchakato huo.

Kulingana na Tutuba, utaratibu huo unalenga kuwaondolea watalii usumbufu wa kutafuta huduma za kubadilisha fedha pindi wanapofika Tanzania.

"Wakati mwingine wageni hawa hufika siku za sikukuu au hata wikiendi wakati maduka haya yamefungwa, uwepo wa maduka haya ndani ya hoteli hizi kutaondoa usumbufu na changamoto za aina hiyo," amesema Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania.

Uamuzi huo unalenga kudhibiti biashara zisizo rasmi za kubadilisha sarafu ya Marakeni nchini Tanzania./Picha: Getty

Kauli ya Tutuba inakuja pia wakati Serikali ikitoa onyo kali kwa baadhi ya watu wanaoendelea kuhodhi na kuficha sarafu za Kimarakeni na kufanya mzunguko wake kwenye soko kuendelea kuwa mdogo.

Kulingana na Tutuba, wafanyabiashara hao wako katika nafasi kubwa ya kupata hasara kulingana na mabadiliko ya mara kwa mara ya uchumi wa kidunia.

Sio Suluhisho Sahihi

Hata hivyo, kwa mujibu wa wadau katika sekta ya Utalii na Maliasili, uanzishwaji wa maduka ya fedha ndani ya hoteli za hadhi ya nyota 3 hadi 5 nchini Tanzania, sio mwarobaini wa tatizo lenyewe.

Wadau hao wanasema kuwa uamuzi huu unaweza kuwa mzigo zaidi kuliko suluhu ya kutatua uhaba mkubwa wa dola za Kimarekani nchini Tanzania.

"Tunadhani ipo haja ya msingi kufanya tathmini ya athari za udhibiti na tathmini ya athari za kiuchumi kabla ya utekelezwaji wa maamuzi haya," Kennedy Edward, ambaye pia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Hoteli Tanzania (HAT), anaiambia TRT Afrika.

Edward anasema sekta ya maliasili na utalii ni sekta ya kihuduma na hivyo uamuzi huo utaathiri uwekezaji moja kwa moja, badala ya kupata suluhu ya tatizo lenyewe.

Kwa mujibu wa Afisa Mtendaji Mkuu wa HAT, malipo yote ya huduma za Maliasili na Utalii hufanywa kimtandao na hauhusishi malipo ya moja kwa moja, akiwa na maana fedha taslimu.

"Kupitia uamuzi huo, mdhibiti anataka mtalii aingie kwenye maduka haya ili avunje dola kwa shilingi, kitu ambacho hakifanyiki katika sekta hii," anaelezea.

Wamiliki wa hoteli za kitalii zenye hadhi ya kati nyota 3 hadi 5, kuanzisha maduka ya kubadilishia fedha ndani ya hoteli hizo./Picha:Getty

Gharama kubwa za Uendeshaji

Kulingana na Edward, uamuzi wa aina hiyo utaongeza gharama za uendeshaji biashara, kwani mchakato huo utahusisha kuajiri wafanyakazi na ubadilishaji wa sarafu hizo.

Mbali na hayo, Edward pia anagusia gharama kubwa za kupata leseni ya kuendesha maduka haya, iwapo kanuni hii itaanza kufanya kazi ifikapo Julai 1, 2024.

Itakugharimu shilingi 1,000,000 (dola 400) kupata leseni ya kuendesha maduka haya, na ada ya mwaka ya 500, 000(dola 200)….hapo bado hujalipa wafanyakazi wa maduka hayo.

Kennedy Edward

Edward anasisitiza haja ya kufanya tathmini ya kina kuona ni namna gani maamuzi haya yataathiri biashara ya hoteli katika sekta yenye kuihakikishia Tanzania, dola bilioni 2 kila mwaka.

Mawazo hayo yanaungwa mkono na Mwenyekiti wa Chama cha Waongoza Utalii nchini Tanzania (TATO), William Chambulo ambaye anasisitiza kuwa malipo ya huduma za kitalii zifanywe kidijiti badala ya fedha taslimu, akionya kuwa baadhi ya watumishi wa hoteli hizo sio waaminifu.

Wazo la kuruhusu wamiliki wa mahoteli ya kitalii kuwa na leseni ya kuendesha maduka ya kubadilishia fedha inaweza kuwa sio mwarobaini wa kukomesha biashara haramu ya fedha za kigeni na inaweza kuhatarisha usalama wao

William Chambulo

Maduka ya kubadilishia fedha yafungwa

Mnamo mwezi Disemba mwaka 2018, Benki Kuu ya Tanzania ilifanya ukaguzi wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni nchini kote na kubaini kuwa mengi hayakidhi matakwa ya kisheria ya biashara hiyo.

Baada ya ukaguzi huo, BOT iliyaandikia maduka hayo kuyataka kutoa maelezo kwa nini yasifutiwe leseni kutokana na ukiukaji huo. Hatua zilizochukuliwa jana zinatokana na tathmini ya taarifa ambazo Benki Kuu ya Tanzania ilizipokea kutoka kwa waendeshaji wa maduka hayo.

TRT Afrika