Serikali ya Tanzania imeendelea kutoka tahadhari kuhusu ugonjwa wa 'Macho mekundu', huku maradhi hayo yakiendelea kusambaa maeneo tofauti nchini humo.
Kulingana na Wizara ya Afya ya nchi hiyo, ugonjwa wa 'Viral Keratoconjunctivitis' umesambaa kwenye mikoa 17 ya Tanzania, msisitizo ukiwekwa kwenye kuzingatia kanuni bora za usafi.
Mkurugenzi wa Tiba kutoka Wizara ya Afya, Profesa Pascal Ruggajo anasema kuwa dalili za ugonjwa huo zimeanza kushuhudiwa kwenye mikoa ya Singida, Katavi, Kilimanjaro, Mara na Iringa.
Maeneo mengine yalioathirika ni pamoja na Njombe, Ruvuma, Simiyu, Mtwara, Lindi, Songwe, Rukwa na Mwanza.
"Kusambaa huku kumesababisha idadi ya wagonjwa kuongezeka kutoka 1,109 na kufikia 5,359 huku mkoa wa Dar es Salaam peke yake, idadi hiyo ikiongezeka na kufikia 4,792 kutoka 869 ndani ya wiki mbili," anasema Profesa Ruggajo.
Kwa mujibu wa Profesa Ruggajo, Serikali ya Tanzania inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa ugonjwa huo.
Wizara ya Afya pia inasisitiza suala la usafi kama jambo muhimu katika kuzuia maambukizi kusambaa kwa wengine kwani ugonjwa huo husambaa kwa kasi.
Wataalamu wa afya pia wanawaasa Watanzania kuacha kutumia dawa zisizo rasmi, na zisizopendekezwa na madaktari kwa wakati huo na kutotumia dawa za macho zilizotumika na mgonjwa mwingine.