Wizara ya Afya nchini Kenya imesema haina uwezo wa kuajiri madaktari wanafunzi wote kwa sasa.
Wataalamu wa afya walifanya maandamano mbele ya ofisi za Wizara hiyo jijini Nairobi, 9 Julai 2024 na wengine hata wakaamua kukesha nje ya ofisi hizo wakidai kuwa madaktari wanafunzi lazima wapewe nafasi za kazi.
Waziri wa Afya Susan Nakhumicha katika taarifa amesema kuwa kwa sasa serikali haina uwezo wa kutoa ajira kwa wataalamu 3760 wa afya ambao hawajapata nafasi za kazi.
Wataalamu wa afya walifanya mgomo wa siku 56 ambao ulipekea kufanyika kwa makubaliano kati ya serikali na muungano wa wataalamu wa afya 8 Mei 2024.
Suala nyeti katika majadiliano kati ya pande mbili hizo lilikuwa ni malipo ya madaktari wanafunzi.
Mahakama ilitoa mapendekezo kadhaa ya kutatua mvutano kati ya serikali na shirika la wataalamu wa afya.
"Kutumia fedha zilizotolewa mwaka 2024/2025 na kuwapa nafasi madaktari wnafunzi kwa vikundi vikundi huku majadiliano yakiendelea baina ya serikali na uongozi wao, Wizara inaweza kutoa nafasi kwa wanafunzi madaktari 552," Nakhumicha amesema katika taarifa.
Mahakama pia ilitoa pendekezo la kuzingatiwa kuwa wote wanaongoja nafasi wapewe lakini kwa malipo ya Ksh70,000 kwa mwezi kulingana na maagizo ya Tume ya Taifa ya Malipo na Mishahara.
Awali, Muungano wa Madaktari nchini Kenya umependekeza kuwa kila daktari mwanafunzi alipwe 206, 400 kila mwezi.
Wizara ya Afya inasema kwa sasa madaktari wanafunzi wanaohitaji kupewa nafasi ni 3760 kwa bajeti ya bilioni 4.8 .
"Kulingana na bajeti Wizara ya Afya ilipokea shilingi bilioni 3.7 kwa mwaka 2024/2025 ya kulenga kuwalipa madaktari wanafunzi,"
Wizara inasema tangu Januari 2023 imetoa nafasi za kazi kwa madaktari wanafunzi 4,156 wakiwemo maafisa wa afya, wafamasia, madaktari wa meno, wauguzi, na maafisa wa kliniki.