Wizara ya Afya imewataka wananchi kutoa taarifa kwa simu ya dharura ya 199 iwapo watashuku mtu yeyote kuwana maambukizi hayo./ Picha : Reuters 

Wizara ya afya nchini Tanzania imeondoa hofu yoyote ya maambikizi ya Mpox nchini humo kufuatia minong'ono iliyozuka kwa wiki kadhaa nchini humo.

''Wizara ya Afya unautaarifu umma kuwa mpaka sasa Tanzania ni salama na hakuna mgonjwa yeyote aliyepatikana na ugonjwa huo,'' imesema taarifa ya Wizara ya Afya.

Hata hivyo wizara hiyo imesema kuwa inaendelea kufuatilia kwa makini visa vinayoripotiwa na nchi jirani zinazopakana na Tanzania na itashauri umma iwapo loloye litabadilika.

Wananchi wametakiwa kujifahamisha juu ya mwenendo wa ugonjwa wa Mpox uliojulikana mwanzoni kama 'Homa ya Nyani'.

Miongoni mwa dalili zake ni upele, malengelenge, vidonda kwenye mwili, hasa mikononi na miguuni, kifuani, usoni n awakati mwingine sehemu za siri. Dalili zingine ni homa, maumivu ya kichwa, misuli uchovu na kuvimba mitoki.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya wizara ya afya, Kuanzia Mei 2022, ugonjwa huu ulipoanza na kufikia Mei 2024, wagonjwa 97745 na vifo 203 vimeripotiwa kutoka nchi 116 duniani.

''Ugonjwa huu haujaingia nchini, hivyo ni vyema tukashirikiana kuhakikisha nchi yetu inabaki kuwa salama,'' imeendelea kusema taarifa hiyo.

Wizara ya Afya imewataka wananchi kutoa taarifa kwa simu ya dharura ya 199 iwapo watashuku mtu yeyote kuwana maambukizi hayo.

TRT Afrika