Wekeza zaidi katika afya, UNAIDS inaziambia serikali

Wekeza zaidi katika afya, UNAIDS inaziambia serikali

UNAIDS inasema vita ya kimataifa dhidi ya UKIMWI yanadorora
  Mwezi Februari mwaka huu Nchi 12 za Afrika zilijitolea kukomesha UKIMWI kwa watoto ifikapo 2030. / Photo: Getty Images

Mpango wa Umoja wa Mataifa kuhusu UKIMWI (UNAIDS), unakadiria kuwa nchi zilizo na kipato cha chini na cha kati zitahitaji dola za Marekani bilioni 29 kila mwaka ili kufikia malengo ya kukomesha UKIMWI kama tishio la afya ya umma ifikapo mwaka 2030.

"Ni wakati mwafaka sasa kuzikumbusha serikali, taasisi za kimataifa kama benki ya dunia na IMF, kwamba huwezi kusimamisha uwekezaji kwenye ugonjwa kama UKIMWI kwa sababu unaathari kubwa," Winnie Byanyima Mkurugenzi Mkuu wa UNAIDS alisema.

UNAIDS inasema kuwa barani Afrika, maambukizi mapya sita kati ya saba kati ya vijana wenye umri wa miaka 15-19 yalikuwa miongoni mwa wasichana.

Wanawake na wasichana walichangia asilimia 62 ya maambukizi mapya ya virusi hivi, mwaka 2021. Inasema ni asilimia 50 tu ya watoto wanaoishi na ukimwi walipata matibabu ya kuokoa maisha wanayohitaji.

Shirika hilo limezindua ripoti kutokana na utafiti uliofanyika katika nchi 13 za Afrika.

Ripoti hiyo iliyopewa jina la ‘Gawio Tatu: Kufadhili kikamilifu mwitikio wa ukimwi katika Afrika’ ,inahimiza serikali kuangalia afya kama kipengele muhimu katika maendeleo ya kijamii ya kiuchumi na kisiasa ya nchi yoyote.

Kulingana na utafiti huo, janga la Uviko-19, janga la kibinadamu linalo sababishwa na migogoro, pamoja na athari mbaya za mabadiliko ya hali ya hewa ni baadhi ya masuala ambayo yamelazimisha serikali kuelekeza fedha ambazo zingetumika kupambana na magonjwa hayo.

Katika mkutano wao mwezi Februari 2023, jijini Dar es Salaam,nchini Tanzania, mawaziri na wawakilishi kutoka nchi 12 za Afrika walijitolea, na kuweka wazi mipango yao, kukomesha UKIMWI kwa watoto ifikapo 2030.

TRT Afrika