Waziri wa Afya Uganda Dkt.Ruth Aceng ametetea mbele ya Bunge umuhimu wa pendekezo la Serikali la kukopa kiasi cha Dola za Marekani Milioni 18.09 (zaidi ya UGX65.9 bilioni) kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Afrika yaani African Development Fund, ili kufadhili upanuzi na ununuzi wa vifaa vya Taasisi ya Saratani ya Uganda.
Waziri huyo ameongeza kusema kuwa mkopo huo utaboresha huduma ya saratani nchini Uganda na kusaidia punguza mzigo wa kazi ambao madaktari wa saratani wanapambana nao.
Aliyasema hayo alipokuwa mbele ya Kamati ya Bunge ya Uchumi wa Taifa na kubainisha kuwa mradi huo ni sehemu ya mradi wa kuhimiza ujuzi na ustadi katika kanda ya Afrika Mashariki.
Chini ya mpango huu Uganda ilikuwa iongoze uwekezaji katika masuala ya matibabu ya saratani huku Tanzania na Kenya zikiongoza katika masuala ya magonjwa ya Moyo.
Lakini amedai kuwa mradi wa Uganda ulitatizwa na athari za janga la Uviko 19 na kusababisha hitaji la rasilimali za ziada.
"Madaktari ni wachache sana na wamezidiwa na kazi. Unapoingia ndani ya Taasisi ya Saratani ya Uganda leo, kuanzia mlangoni, sehemu za kupitia, na hata karibu na vyumba vya kuosha, kuna wagonjwa," Dkt. Aceng amesema.
"Katika nchi vyengine, hawafanyi kazi kama hiyo. Utakuwa na daktari mmoja anayehudumia mgonjwa 1 au 2 kwa siku, hawa wanaona wangapi kwa siku! Kwa idadi kubwa, mtu yeyote angechoka na asifanye haswa, kile ungetaka kufanya," alielezea Dkt. Aceng.
Amesema ni kwa sababu hiyo, kuna haja ya kuwekeza katika kutoa mafunzo kwa wataalamu wengi wa matibabu ya saratani, lakini pia kuwaajiri na pia kuwalipa vizuri zaidi.
Henry Musasizi, Waziri wa Fedha wa Nchi akionyesha msisitizo kwa kauli ya Dkt. Aceng aliiambia Kamati ya Bunge kuwa Wizara ya Afya kuomba fedha zaidi kwa ajili ya Kituo cha Saratani ina sababu halali.
Musasizi alieleza kuwa upanuzi wa Kituo cha Saratani ulipangwa kuchukua miezi 24, hata hivyo, kutokana na athari za janga la Uviko19, na changamoto za kutoa pesa kwa wakandarasi, utekelezaji wa shughuli za kazi za umma zilizocheleweshwa kwa miezi 18.
Kwa hiyo, mkataba wa kazi za kiraia uliongezeka hadi zaidi ya miezi 42 na bei ya vifaa na kazi iliongezeka.