Bunge la Uganda limejadili swala la ufisadi nchini humo huku wabunge wengine wakidai spika na naibu wake ni wafisadi.
"Wewe Naibu Spika (ThomasTayebwa) na Spika (Anita Among) ni miongoni mwa waliotajwa kuwa ni mafisadi, jina lako limetajwa kuwa mfisadi, pia tunaleta hoja ya kujadiliwa kwa makamishna. Tuna ushahidi wetu na wajitetee, unatuzuia, kuna nini? Unaipeleka wapi nchi hii?" Yorke Alion, mbunge wa Aringa Kusini alisema katika mjadala bungeni.
"Kwa nini msituruhusu kujadili suala la rushwa katika Bunge hili? Hii imezidi, wabunge wote hawa wamepakwa rangi ya wezi," Alion aliongezea.
Mei 2024, Marekani iliwawekea vikwazo maafisa wa serikali ya Uganda watano wa sasa na wa zamani kwa madai kuwa wamehusika katika ufisadi mkubwa au ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu. Spika wa bunge Anita Among ni kati yao.
"Spika wa Bunge Anita Among amewekewa vikwazo kutokana na kuhusika katika ufisadi mkubwa unaohusishwa na uongozi wake wa Bunge la Uganda," taarifa kutoka serikali ya Marekani ilisema.
Hata hivyo, Spika wa Bunge la Uganda amekana tuhuma hizo.
Kwa upande wake, Naibu Spika wa Bunge Tayebwa, alijitetea.
"Bunge limefanywa sura ya ufisadi kwa mfano; 'Sina kazi kwa sababu Bunge linaiba pesa'. Bajeti ya Bunge sio hata 1% ya bajeti ya taifa, kwa hiyo, watu wanashindwa kupata barabara kwa sababu ya Bunge? Je, watu wanashindwa kupata ajira kwa sababu ya Bunge? Je, watu wanashindwa kupata shule kwa sababu ya Bunge? Je, tunashindwa kupata nyongeza ya mishahara kwa sababu ya Bunge? " Tayebwa alihoji.
"Nadhani lazima tukae na kukubaliana kwamba baadhi ya watu wanataka kusimama kwenye misingi ya maadili, halafu Bunge, tunaonekana sisi ni sura ya ufisadi nchini. Na haiwezi kumuacha yeyote kati yetu," Tayebwa amesema.
Mbunge mwengine amesema wananchi wanataka majibu kuhusu tuhuma za ufisadi za viongozi.
Ajenda ya vita dhidi ya ufisadi umekita mizizi nchini humo huku Rais Yoweri Museveni ametangaza vita vikali dhidi ya ufisadi. Rais Museveni alisema kuwa nchi yake inapoteza zaidi ya dola trilioni 1.8 kwa mwaka kwa sababu ya ufisadi.
Tayari mawaziri watatu na katibu mkuu wa wizara wamekamatwa kwa mashtaka hayo.
Naye mwanasheria mkuu amesema kuwa wabunge waache kujilaumu.
"Suala lililo mbele yetu la ufisadi si la upendeleo, ni suala la sisi sote kushughulikia ili tusiingie kwenye siasa zetu ... kwa sababu tutaharibu mapambano yetu dhidi ya ufisadi. Kwa hiyo, tulishughulikie pamoja suala hili la ufisadi, tusiliingize siasa za kivyama," Kiwanuka Kiryowa , Mwanasheria Mkuu wa Serikali amewaomba wabunge.