Uganda itaanda michuano ya AFCON 2027 pamoja na Kenya na Tanzania/ picha Others 

Baraza la Michezo la Taifa (NCS) limeiomba Serikali zaidi ya dola milioni157 (Ugsh bilioni 600 ) kwa ajili ya maandalizi ya shughuli za AFCON 2027.

Baraza hili limeambia bunge kuwa zaidi ya dola milioni 99 (Ugsh 380Bilioni) itakuwa kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Hoima, takriban dola 30 milioni (Ugsh114 Bilioni )kwa ajili ya malipo ya ada za Kujitolea kwa Uganda kuandaa AFCON, huku dola milioni 28 (Ugsh110 Bilioni) zikihitajika kwa ajili ya Ujenzi wa Viwanja 11 vya Mafunzo.

Baraza hili limeambia Kamati ya Bunge ya Elimu na Michezo kwamba viwanja vya mazoezi vya mpira wa miguu vimechaguliwa kwa kuzingatia hali ya vifaa vinavyopatikana na ukaribu na viwanja vikuu vya kuchezea.

Imesema hivi ni pamoja na Viwanja vya Mafunzo ya Namboole, uwanja wa mpira wa Chuo Kikuu cha Kyambogo na Uwanja wa Muteesa 2. Uwanja wa mpira wa Wankulukuku na Chuo Kikuu cha Makerere unahudumia Uwanja wa Kitaifa wa Mandela-Namboole.

Viwanja vya kufanyia mazoezi vya kandanda vilivyo karibu na Uwanja wa Nakivubo ni Uwanja wa Lugogo, Viwanja vya Maafisa wa Kijeshi wa Makindye, Viwanja vya Shule ya Sekondari ya Old Kampala, na Uwanja wa Kadiba.

Uganda imeungana na nchi jirani za Tanzania na Kenya kuanda michuano hii ya soka. Wanaita mradi huu ‘Pamoja,’ Hii itakuwa mara yao ya kwanza kuandaa kombe hilo kubwa zaidi barani kwa mara ya kwanza katika historia ya kombe hilo.

Chachu ya kuandaa mashindano hayo ilizuka 2019, baada ya nchi nne za Afrika Mashariki kufuzu, kwa pamoja, ikiwa ndio mara ya kwanza kabisa katika historia ya kombe hilo kwa Afrika Mashariki kuwa na wakilishi wengi.

Nchi hizi zitalazimika kufanya uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya soka nyumbani ikiwemo kuimarisha viwanja vyao, kuweka sawa usimamizi wa mashirikisho yao ya soka na kuimarisha usalama wa kitaifa ili kuwawezesha kuandaa shindano hilo la kimataifa.

Miongoni mwa masharti yaliyopo ni kuwa viwanja visiwe mbali na uwanja wa ndege, mahoteli makubwa na hospitali kubwa zaidi nchini humo.

Kwa sasa, Tanzania pekee ndio ina uwanja unaotazamiwa kuweza kuandaa kombe hili, lakini itahitaji viwanja zaidi. Ndio maana itakuwa rahisi zaidi kwa nchi hizi kuandaa kwa pamoja.

TRT Afrika