Rais Yoweri Museveni alisema Jumamosi kwamba Uganda ilipoteza wanajeshi 54, akiwemo kamanda, wakati wanamgambo wa al-Shabaab waliposhambulia kambi ya kikosi cha kulinda amani cha Uganda nchini Somalia -- ikiwa ni mara ya kwanza nchi hiyo kutambua idadi ya wanajeshi waliouawa na kundi hilo la kigaidi.
"Askari wetu walionyesha ujasiri wa ajabu na kujipanga upya, na kusababisha kukamatwa tena kwa kambi hiyo. Tuligundua maiti za wanajeshi hamsini na wanne walio fariki, akiwemo Kamanda,” Museveni alisema katika taarifa yake.
Alisema makosa yaliyotokea Somalia yalifanywa na makamanda wawili ambao waliwaamuru wanajeshi hao kurudi nyuma. Alisema makamanda hao wawili wamekamatwa na watakabiliwa na mashtaka katika mahakama ya kijeshi.
Al-Shabab walishambulia kambi hiyo tarehe 26 Mei ambayo ni ya Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) kinachosimamiwa na wanajeshi wa Uganda huko Bulamarer, kilomita 130 (maili 83) kusini magharibi mwa mji mkuu wa taifa wa Mogadishu. Kundi hilo lilidai kuwa shambulio hilo liliua wanajeshi 137 wa Uganda.
Museveni alisema kundi hilo lilijaribu mashambulizi mengine mabaya dhidi ya Baraawe, lakini vikosi vya Uganda viliwapatia pigo kubwa lililowalazimu kukimbia.