Shule ya upili ya Dagoretti jijini Nairobi ilichangamshwa na ugeni usio kifani.
Maelfu ya wanafunzi, walimu, wazazi na wageni wengine wapendao uigizaji na densi walikusanyika katika tamasha la kila mwaka linaloaminiwa kuonyesha tamaduni za makabila na jamii mbalimbali za nchi.
Wanafunzi hushindana katika kucheza densi za kiasili huku wengine wakionyesha vipaji vyao katika uigizaji jukwaani kwa lugha mbali mbali kama Kiswahili, Kiingereza na hata Kifaransa.
''Madhumuni ya tamasha hili ni kukuza vipaji vya wanafunzi huku wakitambulishwa kwa mila na tamaduni mbali mbali zinazoliunda taifa la Kenya,'' anasema mwalimu Rono, wa somo la Kifaransa na mratibu wa klabu ya uigizaji katika shule ya The Kenya High. '' Hapa ndipo wanafunzi wengi wanagundua kuwa utofauti wa kabila na mila ndio fahari ya nchi na sio sababu ya kuwatenganisha,'' anaambia TRT Afrika.
Tamasha hili lilizinduliwa mwaka 1959 kama hafla ya shule nyakati za ukoloni likijumuisha uigizaji hasa wa jukwaani kutoka vitabu vya Waingereza. Hata hivyo, maandalizi ya tamasha hilo yamepanuka na kukua katika miaka iliyofuata likichukua taswira ya Kiafrika na lengo la kukuza utamaduni huu kwa wanafunzi.
Kufikia miaka ya themanini Wizara ya Elimu ambayo ndio muandaaji wake, ilijumuisha matamasha ya shule za msingi, sekondari na vyuo katika tamasha moja kubwa kitaifa.
''Ninaona tamasha kuwa jukwaa bora la kuunda sanaa, kufanya mazoezi na kukuza vipaji vya vijana,'' anasema Henry Wanjala, mkufunzi wa densi za kitamaduni nchini Kenya. ''Hutoa nafasi kwetu kueleza masuala yanayoathiri mfumo wa ikolojia wa kijamii na kiuchumi,'' Henry anaelezea TRT Afrika.
Wizara ya Elimu hutumia fursa hii kumulika masuala mbali mbali katika jamii ambapo wakufunzi huagizwa kuainisha utunzi wao na mada maalumu iliyotengwa.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni ''kufungua fursa za mabadiliko ya kiuchumi ya kijamii''.
Kwa mujinu wa takwimu za Wizara ya Elimu, zaidi ya wanafunzi milioni tatu hushiriki tamasha hili kila mwaka, mbali na washiriki maalumu na wageni wanaohudhuria katika ngazi tofauti.
Fursa ya taaluma na ajira
Takriban watangazaji maarufu wote nchini Kenya wanahusisha vipaji vyao na tamasha hili la shule.
Kuanzia watangazaji wa redio na televisheni na waandishi maarufu wa magazeti na hata waigizaji waliofuata mkondo huo na kuweza kujipatia pato kimaisha.
Tamasha hili limekuwa chanzo kizuri cha kutambua vipaji ambapo baadhi wanachukua masomo ya juu yanayoendana na vipaji vyao na kuwapa ajira baadaye maishani.
Chachu ya kukaa shuleni
Wanafunzi wengi wanalisubiria kwa hamu kuanza kwa tamasha hili kila mwaka.
''Ukifika muda wa tamasha najua nakutana na wanafunzi wengi kutoka shule mbali mbali kote nchini. Unakutana na rafiki au hata ndugu wanaosoma shule tofauti na pia unapata marafiki wapya,'' anasema Oduor, mwanafunzi wa shule ya vijana Magharibi mwa Kenya.
Mbali na ushindani unaokuza talanta zaidi, tamasha hili pia huwatia watoto hamu zaidi kukaa shuleni.
''Kusema kweli wakati mwengine shule inachosha. Unatamani kupata kitu kinachokupumbaza baada ya masomo magumu,'' anasema Oduor. '' Nikijua kuna mazoezi ya uigizaji kwa ajili ya maandalizi ya tamasha ninakuwa na hamu sana kukaa shuleni,'' anaongezea.
Kwa zaidi ya miaka 65 wanafunzi wa shule kuanzia chekechea hadi vyuo nchini Kenya wamekuwa wakishiriki shindano la kila mwaka la muziki na densi za kitamaduni kutoka jamii mbalimbali.
Shule zote zimegawanywa kieneo, ambapo washiriki wanashindana kisha wanaofuzu wanashindana katika ngazi ya mikoa na hatimaye washindi kutoka huko wote wanakutana katika jukwaa la Kitaifa, ambalo kila mwaka huhamishwa miji mbali mbali.
Mwaka huu shindano la kitaifa litakuwa mjini Embu, Mkoa wa Mashariki.