Serikali ya Kongo na CENI zilikataa madai kwamba kura ilikumbwa na machafuko. / Picha: AFP

Umoja wa Afrika, ambao ulifanya kazi ya uchunguzi, ulisema uchaguzi huo ulifanyika katika hali ya utulivu lakini ulibaini changamoto kubwa za vifaa.

Mabalozi wa nchi za magharibi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wametoa wito wa amani mnamo Jumamosi baada ya viongozi wa upinzani kutaja uchaguzi wa Disemba 20 kuwa "ulaghai," huku wengine wakitaka ufutwe.

Balozi 12 za Ulaya pamoja na Ubalozi wa Canada, zimeomba utulivu katika mji mkuu Kinshasa.

"Ikiwa bado shughuli ya kuhesabu kura inaendelea, tunatoa wito kwa vyama vyote vinavyohusika... ili kuonyesha utulivu," waliandika.

Haya yanajiri baada ya viongozi watano wa upinzani, kupitia taarifa ya pamoja, kuitisha maandamano siku ya Jumatano wiki ijayo.

Wagombea wa urais hao ni pamoja na Dk wa magonjwa ya wanawake Denis Mukwege, mshindi wa tuzo ya Amani ya Nobel 2018; na mtendaji wa zamani wa shirika la mafuta Martin fayulu.

"Tutafanya maandamano dhidi ya yaliyobainishwa wakati wa shughuli za upigaji kura," waliandika katika barua kwa gavana wa Kinshasa, ambapo wanapanga kufanya maandamano hayo.

Wagombea wengine watano wa upinzani, wakiwemo mfanyibiashara na gavana wa zamani Moise Katumbi, walitoa taarifa tofauti wakitaka kura hiyo ifutwe, wakisema imeharibiwa na "udanganyifu mkubwa."

Ubalozi wa Marekani pia ulitoa wito kama huo wa kutaka hali ya utulivu siku ya Ijumaa.

Takriban raia milioni 44 katika taifa hilo la watu milioni 100 walijiandikisha kupiga kura, huku zaidi ya wagombea 100,000 wakiwania nafasi mbalimbali.

Rais Felix Tshisekedi, mwenye umri wa miaka 60, anawania tena nafasi ya urais dhidi ya wagombea 18 wa upinzani. Tshisekedi anapigiwa upatu kushinda uchaguzi huo wa urais haswa ikizingatiwa kuwa upinzani umegawanyika.

Aidha, afisa mmoja wa uchaguzi alisema kuwa upigaji kura uliochelewa unaendelea katika maeneo machache mashariki ya mbali ya nchi hiyo umeidhinishwa Jumapili.

Macaire Kambau Sivikunula, afisa wa uchaguzi katika mkoa wa Kivu kaskazini mashariki mwa nchi, aliiambia AFP kuwa Tume ya uchaguzi CENI imetoa ruhusa maalum kwa vituo vitano vya kupiga kura kufunguliwa siku ya Jumapili kwa wapiga kura.

Tume ya Uchaguzi nchini humo, CENI, iliongeza rasmi muda wa kupiga kura hadi Alhamisi kwa vituo ambavyo havikuweza kufunguliwa siku ya upigaji kura.

Lakini bado kura zilikuwa zikipigwa Jumamosi katika maeneo ya mbali, kulingana na baadhi ya maafisa, ikiashiria matatizo yanayoendelea.

Mnamo Ijumaa jioni, CENI ilitoa matokeo ya urais kutoka kwa raia wa Kongo wanaoishi ngambo, ambayo inawakilisha sehemu ndogo ya wapiga kura, ikionyesha uongozi wa muda kwa Tshisekedi.

Hata hivyo, matokeo yaliyoratibiwa kutangazwa Jumamosi yaliahirishwa hadi Jumapili.

Matokeo ya majimbo 26 ya DRC yanatarajiwa kuanza kutolewa baadae.

Tume ya uchaguzi ya CENI pia imetangaza kuanzisha uchunguzi dhidi ya "vitendo vya vurugu, na uharibifu uliofanywa na wagombea fulani wenye nia mbaya."

AFP