Kampeni zimeisha rasmi nchini DRC, sehemu kubwa ya nchi imegubikwa na hali ya utulivu huku raia wake wakisubiri kwa hamu siku ya kupiga kura. Picha/TRT Afrika. 

Hamisi Iddi Hamisi

TRT Afrika, Kinshasa, DRC

Uchaguzi mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) unaofanyika Disemba 20 mwaka huu ni moja ya chaguzi zinazotikisha zaidi mwaka 2023 na kufuatiliwa kwa karibu nchini DRC na hata nchi jirani na barani Afrika kwa ujumla.

Panda shuka za amani na hali ya usalama DRC zimeonesha kutetereka kwa uwezo wa jeshi la serikali katika kukabiliana na vikundi vya waasi katika maeneo mbali mbali ya nchi. Hivyo, kusababisha hali ya usalama kutoweka na watu wengi kukimbia makazi yao ya kudumu na kuingia uhamishoni katika nchi jirani au kuhamia miji mingine.

Kundi hili la wakimbizi wa ndani kwa namna moja inaweza kusemwa ya kwamba wamenyang’anywa haki yao ya kidemokrasia kwani hawatoweza kupiga kura kwa sababu wamelazimika kuhama maeneo yao ambayo walijiandikisha.

Mbali na kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2018 uligubikwa na ghasia na madai ya udanganyifu wa hapa na pale, Rais anayemaliza muhula wa kwanza Felix Tshisekedi ni mmoja ya wagombea 26 watakaochuana kukalia kiti cha urais wa taifa hilo.

Tume Huru ya Uchaguzi CENI imesema walemavu watapewa kipaombele ili waweze kupiga kura kwa haraka na wepesi. Picha/TRT Afrika. 

Tishio la upinzani kwenye kinyang’anyiro cha urais

Tshisekedi na chama chake tawala cha UDPS anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wagombea kama Martin Fayulu, waziri mkuu wa zamani na mwanasiasa mkongwe anayetegemea kuwa safu ya mbele katika kambi ya upinzani dhidi ya Tshisekedi.

Mmiliki wa TP Mazembe, klabu kongwe ya mpira wa miguu maarufu na yenye mafanikio makubwa kwenye historia ya soka nchini DRC na Afrika kwa ujumla, Moise Katumbi anategemea kutumia uzoefu wake wa uongozi kama Gavana wa Katanga aliyepita kushika uongozi wa nchi kama rais iwapo atashinda uchaguzi kupitia chama alichokianzisha mwaka 2018 cha Ensemble.

Katumbi anajaribu kutumia ushawishi wake mkubwa kwenye michezo na biashara ili kuwashawishi wananchi wampe kura za kutosha na hatimaye aongoze taifa hilo lenye rasilimali nyingi zaidi kuliko nchi yoyote ile Afrika.

Raia wa DRC wanasema wataitumia vyema haki yao ya kupiga kura. Picha/TRT Afrika. 

Wakati umefika wa DRC kuongozwa na mwanamama

Kati ya wagombea hao 26 kuna wanawake wawili wanaowania kiti cha urais. Marie Josee Ifoku (58) maarufu, ‘‘Mama wa fagio’’ hii ni mara yake ya pili kushiriki uchaguzi kama mgombea wa urais. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2018. Ifoku anaweka wazi uwezo wake na tajiriba aliyoipata mwaka 2018 kuwa imemfunza na itamsaidia kushinda mwaka huu.

‘‘Mwaka wa 2018 sikujiandaa vizuri, lakini nilipata jukwaa na fursa kuonekana. Nimezingatia mengi na kupata uzoefu. Ndio maana sikuvunjika moyo, mara hii nimejizatiti na ninaamini nitafanya vizuri zaidi.’’ Ifoku alinukuliwa kwenye moja ya mahojiano yake.

Akiongea na TRT Afrika katika mahojiano maalum Marie Josee Ifoku amesema, ‘‘Katiba ya DRC ya mwaka 2006 inampa mwanamke asilimia 50 katika usimamizi wa mambo ya umma. Lakini hali halisi haioneshi hivyo.’’

‘‘Hivyo tunampa nafasi mwanamke katika siasa kwa mujibu wa sheria, mwanamke lazima aendelee kupigania haki yake,’’ Ifoku aliongeza.

Swali la kujiuliza hapa ni je, wanawake watampa kura za kutosha mwanamama huyu anayetaka kuisuka DRC mpya iliyo safi na yenye utawala bora?

Tayari mgombea mwanamke mwenzake Joelle Belle ametangaza kujitoa kama mgombea na kumuunga mkono rais Tshisekedi.

DRC ni moja ya nchi zenye rasilimali nyingi barani Afrika na duniani kote. Lakini sehemu kubwa ya raia wake bado hawajanufaika na utajiri huo kutokana na migororo isiyokwisha. Picha./TRT Afrika. 

Machungu ya wanawake wa DRC na werevu wa vijana wa leo

Wanawake nchini DRC wanasema wamepitia unyanyasaji na hali ya juu kwa muda mrefu. Katika miongo hiyo kumekuwa na watetezi wa muda wanaokuja na kuondoka ambapo hitajio lao hasa la kuishi kwa amani na usalama limekuwa ni donda sugu.

Bila shaka wanahitaji mtetezi anayewafahamu zaidi, lakini mwenye maono mbali ya atakayeleta mabadiliko katika jamii nzima ya wakongomani.

Wakizungumza na TRT Afrika mjini Kinshasa, wasichana na vijana wahitimu wapya katika sekta mbali mbali wamesema wanatambua utajiri uliopo nchini mwao, lakini wanashangazwa kuona maisha ya walio wengi ni duni. Wanaamini mabadiliko yanaanza katika kumchagua kiongozi mzuri mwenye nia thabiti ya kuijenga DRC vilivyo kupitia rasilimali zake.

Mwanaharakati kijana wa kike Natalie Maliva anasema, ‘‘Ikiwa tutawapigia kura watu wema hali yetu ya maisha itaboreshwa. Kwa upande mwingine, ikiwa tutawapigia kura watu wabaya mabadiliko yatakuwa mabaya.’’

Shauku kubwa ya vijana nchini DRC ni kutaka kuona viongozi wanaowachagua wanaleta mabadiliko ya kweli. Picha/TRT Afrika.

Kutokomeza makundi ya waasi na kurudisha usalama

Raia wengi wanaonesha wanataka mabadiliko ya mwenendo wa nchi hasa katika suala zima la usalama. Wanataka migogoro na makundi ya waasi kama ADF na M23 imalizwe kabisa.

Kufanikisha hili ndio maana moja ya manifesto za chama tawala UDPS ni ‘‘usalama’’ na ‘‘maendeleo.’’ Hii inaonesha sauti za wananchi kutaka amani na usalama zinafikia viongozi wa nchi, lakini swali je kabla ya uchaguzi kuna nini kinazuia hali ya usalama isiletwe?

Ni baadhi ya maswali wanayohoji watu wanaoweza kudhaniwa kuwa ni wapinzani lakini wao wanasema ikiwa sasa hakuna kinachofanyika basi hata baada ya uchaguzi hakuna kitakachofanyika.

Kinshasa ndio inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wapiga kura milioni 5. Picha/ TRT Afrika. 

CENI iko tayari kusimamia uchaguzi, usalama upo?

Kwa ujumla, kuanzia jiji la Kinshasa na majimbo yote 26 ambayo zoezi la upigaji kura litafanyika amani imetawala. Tume huru ya uchaguzi nchini DRC (CENI) imesema vitendea kazi vimesambazwa kwenye vituo vya kupigia kura, na Umoja wa Mataifa (UN) umetumia vikosi vyake kusaidia usambazaji wa vitendea kazi hivi hasa kwenye maeneo ambayo yamezorota kiusalama.

Tayari hapo awali Rais Tshisekedi alitangaza kuwa majimbo ya Masisi, Kivu, Kwamouth upande wa Mashariki mwa DRC hayatafanya uchaguzi huu kutokana na kukosekana kwa usalama.

Wapiga kura zaidi ya milioni 40 nchi nzima, katika majimbo 26, Kinshasa ndio inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wapiga kura 5, 062, 991. Huku wastani wa majimbo mengine ukibaki kuwa ni wapiga kura milioni 1.3 kwa kila jimbo.

Tume huru ya uchaguzi imeonya mikusanyiko, kupiga kelele za kushangilia na kampeni siku ya uchaguzi, na imewataka wapiga kura kurejea makwao pindi tu watakvyomaliza kupiga kura.

Asubuhi na mapema saa kumi na mbili kamili vituo vya kupigia kura vitafunguliwa na zoezi litaanza, kisha vitafungwa saa kumi na moja kamili jioni.

Vyombo vya ulinzi na usalama vya serikali vikishirikiana na vya UN viko kwenye doria ili kuhakikisha usalama unapatikana.

Uchaguzi huu unafuatiliwa kupitia wawakilishi wa kimataifa, mashirika, na taasisi za kimataifa. Tayari wajumbe kutoka ukanda wa Afrika Mashariki EAC, na kusini mwa bara la Afrika SADC wamefika ili kufuatilia kwa karibu uchaguzi huu.

Raia wengi wa DRC wana matumanini uchaguzi utakuwa wa haki na huru na utafanyika katika hali ya usalama kabisa. Picha/TRT Afrika. 

Wenye mahitaji maalumu hawajasahaulika

Watu wenye ulemavu na mahitaji maalumu wametengenezewa mazingira rafiki waendapo kupiga kura. CENI imewajulisha wapiga kura wenye ulemavu kuwa watapewa kipaumbele lakini muhimu wafike mapema katika vituo vya upigaji kura.

‘‘Ikiwa mvua itanyesha siku ya Disemba 20, nitachukua mwamvuli wangu na mtoto wangu nitaenda kupiga kura na kufungua njia kwa wapiga kura wengine,’’ mmoja wa walemavu wa miguu jijini Kinshaa aliiambia TRT Afrika.

Ari ya raia wengi wa DRC wana matumanini uchaguzi utakuwa wa haki na huru na utafanyika katika hali ya usalama kabisa.

Dhana ya uchakachuaji wa matokeo kwenye vituo vya kupiga kura inaweza kutia doa zoezi zima la uchaguzi. Picha/TRT Afrika. 

Hofu kuhusu kutetereka kwa amani

Wachambuzi wa masuala ya kidemokrasia wanasema mitazamo imejikita katika kuona ni kiasi gani DRC itauthibitishia ulimwengu kuwa imepevuka kidemkorasia baada ya kuendesha uchaguzi huru na wa haki wa pili tangu kupata uhuru mwaka 1960.

Kampeni zimefungwa rasmi tarehe 18 Disemba na wakongomani wako tayari kuchagua viongozi wao kwa maana ya rais, wabunge wa taifa na wabunge wa jimbo.

Kwa mitazamo ya wengi, pindi upigaji kura utakapomalizika, na zoezi la kuhesabu kura likaanza na ndani ya saa 24 matokeo yasiyo rasmi kuanza kutoka huenda hali hii ikasaidia kutuliza munkari wa wananchi.

Dhana a uchakachuaji wa matokeo kwenye vituo vya upigaji kura unaweza kutia doa zoezi zima la uchaguzi.

Rais Tshiekedi na baadhi ya wagombea wanatarajia kupiga kura kwenye moja ya vituo vya upigaji kura jijini Kinshasa.

TRT Afrika