Ubalozi wa Marekani nchini Kenya umetoa tahadhari ya kusafiri katika maeneo maalumu nchini Kenya kutokana na ongezeko la mafuriko yanayoendelea kukumba maeneo kadhaa ya nchi hiyo.
Katika tahadhari hiyo iliyotolewa siku ya Jumatano, Mei 1, Marekani imewashauri raia wake kuchukua tahadhari pindi wanaposafari katika nchi hiyo au ndani ya nchi. Katika taarifa hiyo, eneo la Maasai Mara na Rift Valley yameorodheshwa miongoni mwa maeneo yaliyoathiriwa zaidi.
"Iwapo unasafari ndani ya Kenya, wasiliana na kampuni yako ya utalii na eneo la malazi kuhakikisha kwamba ni salama kusafiri,” imesoma sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa kuongezea, raia wote wa Marekani wameshauriwa kutoendesha magari wakati mvua kubwa zikiendelea au kusimama pembezoni mwa barabara. Pia wametahadharishwa dhidi ya kuvuka madaraja ambayo yamefunikwa na maji.
Ubalozi wa Marekani umetoa tahadhari ya kusafiri maeneo maalum nchini Kenya masaa machache tu baada ya Ubalozi wa Uingereza kutoa tahadhari ya kusafiri kwa sababu ya mafuriko yaliykumba nchi ya Kenya.
Raia wa Uingereza ambao tayari wako nchini walishauriwa kuepuka kutembea, kuogelea au kupiga mbizi kwenye maji ya mafuriko na pia kupanga safari zao kwa uangalifu huku wakizingatia mwongozo wa wenyeji.
Mafuriko yanayoshuhudiwa nchini Kenya yamehangaisha wakazi na kusababisha hasara kubwa, haswa katika mji mkuu wa Nairobi na kaunti ya Rift Valley.