Wasanii wa Kenya wanashauri kuendelea kuhifadhi muziki na utambulihso wa Kiafrika katika tamasha kama Grammy Picha: Frasha

Na Yusuph Dayo

Frasha sio jina geni katika sekta ya muziki nchini Kenya. Ni msanii wa muziki wa kufoka anayesifiwa sio tu nchini mwake bali hata kimataifa. Ni miongoni mwa wasanii wa Kenya walioanzilisha mfumo wa ‘Genge’, yaani mtindo wao wakenya wa mziki wa kufoka na kizazi kipya.

Ameambia TRT Afrika kuwa amefurahishwa sana japo pia kushangazwa aliposikia habari za tamasha la Grammy kuwatengea Waafrika kitengo chao cha tuzo.

‘‘Sikudhani ningeona siku kama hii maishani,’’ anasema. ‘’Niliota kwa miaka mingi. Kweli tumepigania kwa muda mrefu.’’

Frasha 36, ambaye jina lake kamili ni Francis Amisi, amekuwa na ufanisi mkubwa katika fani ya muziki nchini Kenya, akitoa nyimbo maarufu na wakati mwingine kushirikiana na wasanii wakubwa nchini mwake.

Anasema kuwa hii ni ishara Kamba wasanii wa Afrika wanatambuliwa kimataifa.

‘‘Hii ni siku njema kwa wasanii wa Kenya, na Afrika Mashariki, kwasababu tulipoanza tulitaka tupate utambulisho kimataifa. Afro Beat tayari inajulikana sana, wengi wanaizungumzia. Wanashinda hadi tuzo za Grammy,’’ anasema. ‘‘ Tunataka watu watutambue kama vile wanavyotambua muziki wa Amapiano Afrika Kusini au wa Afrika Magharibi. Ndicho tulipigania.’’

Ni hatua njema

Baadhi ya wasani wa Afrika wamefanikiwa katika ngazi ya kimataifa, hata wakishirikiana na majina makubwa katika muziki. Wengi wanaona hii kama njia ya kuwapenyeza katika ngazi ya juu kimuziki huku tuzo kama ya Grammy ikichukuliwa kuwa ndio kilele.

Lakini sio rahisi kwa waafrika kujinyakulia nafasi katika tuzo hizo.

Tamasha hilo la Grammy limekuwa likishutumiwa kwa ubaguzi katika njia wanazogawa tuzo hizo.

Inaaminiwa kuwa asili mia kubwa ya muziki unaovuma zaidi kimataifa unatoka kwa wasanii weusi na wa kilatina. Hata hivyo wao ndio wanaopokea tuzo chache zaidi katika tamasha hilo.

Na ni wasanii wachache sana wa kiafrika waliopata chochote akiwemo Miriam Makeba, ambaye ndiye mwanamke wa kwanza wa kiafrika kushinda 1966, kufuatia albamu yake, ‘An evening with Belafonte’.

Taasisi hiyo kubwa zaidi ya muziki duniani imekuwa ikijaribu kukomboa sura yake hasa katika miaka ya hivi majuzi baada ya kupokea shutuma kali kutoka kwa wasanii na mashabiki wao.

Ni wazi kuwa hatua kama hii ya juzi kuwapa waafrika kitengo chao cha tuzo, ni miongoni mwa juhudi za kujisafisha na kurudisha Imani kwa tamasha hilo.

Katika kitengo hiki, wasanii wa Afrika watashindana katika mitindo ya “Afrobeat, Afro-fusion, Afro Pop, Alte, Amapiano, Bongo Flava, Genge, Kizomba, Chimurenga, High Life, Fuji, Kwassa, Ndombolo, Mapouka, Drill kutoka Ghana, Afro-House, mzuiki wa hip hop wa Afrika Kusini na Jazz ya Ethiopia.

Kuendeleza utambulisho asili wa kiafrika

Magwiji wa muziki wakikutaja jina basi na wewe utatajika kote barani. Ndivyo wanavyoamini wasanii wengi Afrika.

frasha na kundi lake P Unit walikuwa waazilishi wa muziki wa Genge unaotambulika Kenya  Picha : Frasha 

Japo muziki wa kiafrika unatajika miongoni mwa sauti tamu zaidi pamoja na densi za kuvutia, bado wengi wanategemea kupewa jeki na majina makubwa ili watoke.

Frasha anasema kuwa ni muhimu kuimarisha asili na utambulisho wa utamaduni wakati wa kutafuta umaarufu nje.

‘’Ushauri wangu ni kuwa tushikilie utambulisho wetu. Tusiwe tunaiga vitu vya wengine kwa kuwa wanavuma. Beba chako mwenyewe na usifuate upepo,’’ anasema. ‘’Mara utaona wanakutafuta kwa kile ulicho nacho wewe.’’

Frasha anaamini kuwa mlango umefunguliwa sasa kwa wasanii wapya na anawasahuri waendeleze harakati za waliowatangulia.

‘‘Nataka niwaone hawa vijana wapya wakivunja vikwazo. Wafike mahali ambapo sisi hatukufika. Ndoto yangu niwaone wasanii kama Trio Mio akishirikiana na Rick Ross kutoa muziki, au Wiz Khalifa akimshirikisha Boutross.’’ Amesema.

Miongoni mwa wasanii wa Afrika waliowahi kushinda tuzo za Grammy ni Miriam Makeba, Ladysmith Balck Mambazo, Wiz Kid na Tems pmaoja na wengine.

TRT Afrika