Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania Mobhare Matinyi./Picha: Wengine

Sasa ni rasmi.

Jina la Tume ya Uchaguzi nchini Tanzania (NEC) litabadilika kuanzia Ijumaa Aprili 12, 2024 na kuwa Tume Huru ya Uchaguzi.

Kulingana na taarifa yake kwa vyombo vya habari, Msemaji Mkuu wa Serikali ya nchi hiyo Mobhare Matinyi amesema kuwa chombo hicho kinachoratibu michakato ya uchgauzi nchini Tanzania, sasa litakuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi 'Independent National Electoral Commission', kwa lugha ya kiingereza.

“Tunapenda kuvitaarifu vyombo vyote vya habari kwamba, kufuatia tangazo la Serikali namba 225 la Machi 29, 2024 Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi namba 2 ya mwaka 2024, itaanza kutumika rasmi Aprili 12, 2024," sehemu ya taarifa hiyo ilisema.

Uamuzi huo unakuja miezi minne baada ya wadau wa vyama vya siasa nchini Tanzania kutaka mabadiliko ya Sheria ya Uchaguzi wa nchi hiyo

.

Hata hivyo, muundo wa tume hiyo mpya bado haukawekwa wazi.

Hatua hii inakuja wakati Tanzania inatarajia kuingia katika uchaguzi mdogo wa Serikali za mitaa baadaye mwaka huu na kutoa fursa ya kufanyika kwa uchaguzi Mkuu wa kitaifa utakaohusisha mihimili ya bunge na Utawala, ifikapo Oktoba 2025.

TRT Afrika