Na Brian Okoth
Felix Tshisekedi, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, amemteua Waziri wa Mipango Judith Tuluka Suminwa kuwa waziri mkuu mpya wa nchi hiyo.
Hii ni mara ya kwanza katika historia ya DRC kwa mwanamke kushika wadhifa wa waziri mkuu. Nchi hiyo imekuwa na mawaziri wakuu 29 tangu uhuru mnamo Juni 1960.
Msemaji wa Tshisekedi alisema kwenye televisheni ya taifa siku ya Jumatatu kwamba uteuzi wa Suminwa unaanza mara moja.
"Ninajua kuwa kazi ni kubwa na changamoto (ni) kubwa, lakini kwa kuungwa mkono na rais na kila mtu, tutafika," Suminwa alisema katika mkutano na waandishi wa habari Jumatatu baada ya kuteuliwa.
Changamoto kuu
Ukosefu wa usalama, haswa katika eneo la mashariki mwa DRC, itakuwa moja ya changamoto kuu ambazo waziri mkuu mpya atakabiliana nazo.
Suminwa ni mwanachama wa chama tawala cha Union for Democracy and Social Progress, ambacho kilishinda viti 69 katika Bunge la Kitaifa lenye wabunge 500.
Kwa hivyo, chama hicho kilipata nafasi yake kama chama cha wengi kati ya vyama vingine 44 katika uchaguzi mkuu uliofanyika Desemba 20, 2023.
Suminwa anachukua nafasi ya Jean-Michel Sama Lukonde mwenye umri wa miaka 46, aliyejiuzulu Februari 20 baada ya kuchaguliwa katika uchaguzi wa Desemba kuwa mbunge wa wilaya ya Kasenga.
Lukonde, mtendaji mkuu wa zamani wa kampuni ya madini, alihudumu kama waziri mkuu wa DRC tangu Februari 2021.
Uzoefu
Nchini DRC, ni kinyume cha sheria kwa mtu kuhudumu serikalini na bungeni kwa wakati mmoja. Hii ina maana kwamba waziri aliyechaguliwa bungeni anapaswa kuchagua iwapo atasalia serikalini au kuhudumu bungeni.
Suminwa ana Shahada ya Uzamili katika Sayansi ya Kazi (Utawala na Usimamizi wa Utumishi) kutoka Chuo Kikuu Huria cha Brussels.
Pia ana Shahada ya Kwanza katika Sayansi ya Uchumi Inayotumika (chaguo la Usimamizi wa Fedha) kutoka Vitivo vya Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mons, Ubelgiji.
Aliteuliwa kuwa waziri wa mipango Machi 2023. Kabla ya hapo, alikuwa naibu mratibu anayesimamia masuala ya utawala na uendeshaji wa Baraza la Rais la Kuangalia Mikakati.
Mkuu wa serikali
Ana zaidi ya miaka 20 ya uzoefu wa kimataifa katika utawala wa kidemokrasia na ujenzi wa amani. Pia ana uzoefu katika fedha za umma, hasa kuhusiana na ufuatiliaji wa mageuzi ya bajeti.
Pia amefanya kazi katika Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kama mtaalam wa kitaifa katika mradi wa kusaidia jamii mashariki mwa DRC.
Waziri mkuu wa DRC anaongoza serikali, ambayo pia inaundwa na mawaziri na manaibu waziri.
Nchini DRC, baraza la mawaziri linajulikana zaidi kama serikali.
Majukumu
Waziri Mkuu, ambaye ndiye mwenyekiti wa baraza la mawaziri, pia anamshauri na kumsaidia rais katika utekelezaji wa majukumu aliyokabidhiwa.
Pia anatoa kanuni za serikali na kuteua watumishi wa chini wa serikali na maafisa wa jeshi.
Kabla ya kutangaza hali ya hatari, rais lazima kwanza ashauriane na waziri mkuu na marais wa mabunge yote mawili - Bunge la Kitaifa na Seneti.
Mnamo Januari 20, 2024, baada ya kuapishwa kwa muhula wa pili, Rais Tshisekedi alianza shughuli ya kumtafuta waziri mkuu.
Muungano wa walio wengi
Rais alipaswa kwanza kupata muungano wa wengi katika Bunge la Kitaifa kabla ya waziri mkuu kutajwa na kuunda serikali.
Nchini DRC, waziri mkuu lazima atoke kwenye chama au muungano wa wengi katika Bunge la Kitaifa.