Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi amemteua kiongozi wa zamani wa wanamgambo Jean-Pierre Bemba kuwa waziri wa ulinzi katika mabadiliko ya serikali, huku taifa hilo likikabiliwa na mzozo wa kivita katika eneo la mashariki mwa nchi.
Bemba, ambaye alihudumu kama makamu wa rais kutoka mwaka wa 2003 hadi 2006, alihukumiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, kwa uhalifu uliofanywa na waasi chini ya amri yake, lakini mwaka wa 2018, mahakama hiyo ilibatilisha hukumu yake.
Atachukua nafasi ya waziri wa ulinzi wa sasa Gilbert Kabanda. Aliyekuwa mkuu wa wafanyikazi wa Tshisekedi, Vital Kamerhe, aliteuliwa kuwa waziri wa uchumi, baada ya kupatikana na hatia ya ubadhirifu na kuhukumiwa kifungo cha miaka 20 jela.
Baadaye aliachiliwa huru mwaka uliofuata. Wateule wote wawili sio wanachama wa Union for Democracy and Social Progress (UDPS), cha rais Tshisekedi.
Uamuzi huo ulikuja huku nchi hiyo ikijiandaa kwa uchaguzi mwezi Desemba mwaka huu ambapo rais Tshisekedi anatarajiwa kugombea tena urais.
Akitangaza uteuzi huo kwenye televisheni ya taifa Alhamisi usiku, msemaji wa rais Tshisekedi alisema mabadiliko hayo ya baraza la mawaziri yalikuwa ‘’muhimu sana’’ kwa nchi kutokana na ‘’utaalamu’’ wa mawaziri wapya walioteuliwa.