Shehena ya kwanza ya chanjo ya Mpox iliwasili Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mnamo Septemba 5, 2024. / Picha: Reuters

Na Sylvia Chebet

Amini usiamini, kuna "maisha ya kijamii ya virusi". Lakini tofauti na viumbe wote ulimwenguni ambao hutafuta utaratibu, jamii hii isiyo ya kawaida na ya uvamizi inasitawi katika machafuko.

Wataalamu wa afya ya umma wanaogopa mchanganyiko huu wa machafuko na kuenea kwa virusi, kama vile hutokea mara nyingi katika sehemu fulani za dunia.

Kitovu cha mlipuko wa sasa wa Mpox, ambao Shirika la Afya Ulimwenguni limetangaza "dharura ya afya ya umma unaotia wasiwasi jumuiya ya kimataifa", ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, nchi inayokumbwa na mzozo wa muda mrefu unaohusisha vikundi kadhaa vya waasi.

Shirika la 'Médecins Sans Frontières" (MSF), pia linajulikana kama Madaktari Wasio na Mipaka, linasema kesi zimeripotiwa katika maeneo yenye watu wengi kama Goma - jiji la watu milioni mbili - na katika maeneo ambayo mamia ya maelfu wametafuta hifadhi kutokana na mgogoro wa silaha unaoendelea Kivu Kaskazini.

"Zaidi ya maambukizi 23 yaliothibitishwa yametoka Kivu Kaskazini katika wiki iliyopita pekee, lakini tunaona ongezeko la maambukizi. Pia kumekuwa na hali ya kuenea kwa maambukizi katika kambi za wakimbizi wa ndani, na maambukizii 11 yamethibitishwa," Agnese Comeli, ambaye anaongoza ukabilianaji wa maradhi ya Mpox ya MSF huko Goma, anaiambia TRT Afrika.

Mlipuko katika kambi zilizojaa watu umeleta hali ya wasiwasi kwa madaktari "Nguzo ya huduma ya Mpox ni kuzuia matatizo kwa kuboresha usafi, kukabiliana na kusambaa kwa virusi, na ufinikaji wa vidonda," anasema Comeli.

Masharti yasiyofaa

Wataalamu wa huduma ya afya wana wasiwasi hasa kwamba masharti ya kuzuia na yanakosekana ndani na karibu na Goma.

"Tunawezaje kutazamia familia zinazoishi katika makao madogo, bila maji ya kutosha, vifaa vya usafi wa mazingira, au hata sabuni, kutekeleza hatua za kuzuia? Je! watoto wenye utapiamlo wanawezaje kuwa na nguvu za kuzuia matatizo?" anashangaa Dk Tejshri Shah, mtaalamu wa magonjwa ya watoto na magonjwa ya kuambukiza katika Shirika la MSF.

Dk Shah pia ana wasiwasi kuhusu viwango vya juu vya unyanyasaji wa kingono unaoathiri wasichana na wanawake wanaoishi katika kambi hizo.

"Wakati wa kikao cha ushauri nasaha ambacho nilihudhuria na manusura wa ubakaji, nilikutana na mwanamke ambaye anaishi na watoto wake saba chini ya karatasi ya plastiki. Mpenzi wake alimtelekeza baada ya kushambuliwa," anaiambia TRT Afrika.

Mtaalamu huyo wa MSF anaona kuwa hatua za kuzuia Mpox ni changamoto kubwa sana kutekeleza katika kambi hizo.

“Kama aliyenusurika kubakwa niliyekutana naye atapata upele kutokana na Mpox, ataambiwa abadilishe nguo zake, afue kila kitu vizuri, ajitenge na kujitenga hadi apone, lakini atafuaje bila sabuni na lita za maji zapatikana kwa uchache tu kila siku?" Anasema Dk Shah.

"Anawezaje kujitenga na kuwalinda watoto wake wakati wanaishi pamoja chini ya makazi yao ya plastiki? Ikiwa atajitenga, ni nani atatafuta chakula cha watoto? Ni nani atakayekusanya kuni? Nani atamfariji mtoto mchanga?"

Msaada wa chanjo

Kuwasili kwa chanjo ya Mpox nchini humo kunatoa taswira ya matumaini kwa DRC iliyokumbwa na migogoro na wataalam wa afya wanaofanya kazi ya kudhibiti mlipuko huo.

Zaidi ya washukiwa 20,000 na maambukizi yaliothibitishwa ya ugonjwa wa ndui na zaidi ya vifo 630 vimerekodiwa nchini DRC, kuanzia Januari hadi Septemba 2024. /Picha: AFP

"Tunafuraha kupokea shehena ya kwanza ya karibu dozi 100,000 za chanjo ya JYNNEOS nchini DRC, pamoja na dozi 100,900 za ziada katika shehena inayofuata," anasema Jean Kaseya, mkurugenzi mkuu wa Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC).

Mwishoni mwa wiki jana, jumla ya dozi 200,000 zilipaswa kupatikana nchini.

Mpox hupatikana katika majimbo kadhaa ya nchi hiyo kubwa ya Afrika ya Kati. Tangu kuanza kwa 2024, wizara ya afya ya DRC imeripoti zaidi ya kesi 4,901 zilizothibitishwa, na takriban vifo 630 vinavyohusishwa na maambukizi hiyo.

Wataalamu wa afya wanasema takwimu hizi zinawakilisha ongezeko kubwa la maambukizi na vifo ikilinganishwa na miaka iliyopita.

Ingawa kusubiri kwa muda mrefu kwa chanjo kumekamilika, upatikanaji hautoshi kukidhi idadi ya watu walio katika mazingira magumu.

"Chanjo ya Mpox iliyopendekezwa na WHO ni ya gharama kubwa, na uzalishaji wake bado hautoshi kukidhi mahitaji mashinani," anaelezea Comeli.

Hatimaye, sio tu chanjo ambazo zitarekebisha tatizo. Wataalamu wa afya wanakiri kwamba kuboresha hali ya maisha ni muhimu katika kupambana na milipuko kama hiyo.

Kumalizika kwa mzozo wa muda mrefu wa kutumia silaha kutamaanisha kwamba wakazi wa DRC waliokimbia makazi yao wanaweza kuondoka katika mazingira machafu katika kambi hizo na kurejea kwenye starehe ya makazi yao, ambapo watakuwa chini ya hatari ya Mpox.

TRT Afrika