Madini ya Tanzanite ambayo ni kito cha buluu kinachovutia yanapatikana kaskazini mwa Tanzania/ Picha: Reuters

Coletta Wanjohi

Istanbul, Uturuki

Tanzania ina madini ya Tanzanite ambayo hayapatikani sehemu nyengine duniani. Madini haya yanasemekana yaligunduliwa mwaka 1967.

Madini ya Tanzanite ambayo ni kito cha buluu kinachovutia yanapatikana kaskazini mwa Tanzania. Migodi ya Mirerani ni sehemu pekee duniani inayozalisha mawe haya ya asilia ya Tanzania.

"Tanzanite inatumika kutengeneza vito vya urembo kama hereni, pete, yaani mtu anaweza kutumia kuchonga vito vya urembo," anaelezea Louisa Katolila, mwanasayansi ambaye ni mtaalamu wa miamba.

Tanzanite ni vito vya kipekee, na inahitaji uzoefu, ustadi na umakini kwa undani katika mchakato wa kukata na kung'arisha. Wataalamu wanasema ni adimu zaidi ya mara 1,000 kuliko almasi.

Tanzanite ina thamani kubwa ikiwa inaweza kuuzwa kati ya dola 100 na zaidi ya dola 500 kwa karati kulingana na ubora/ Picha Reuters 

Rangi tatu tofauti zinaweza kuonekana wakati wa kuangalia madini haya kutoka pembe tofauti- buluu, zambarau na waridi, ambayo yote ni ajabu kutazama.

Tanzanite ya bluu iliyokolea kwa sasa ni miongoni mwa mawe yanayohitajika sana hivyo kuifanya kuwa miongoni mwa vito ghali zaidi duniani.

Lakini kwa nini madini haya yanasemekana kushindwa kuvutia mauzo mazuri licha ya umaarufu wake kwenye tasnia ya vito duniani?

"Kwa maoni yangu naona, sisi Watanzania tunakosa kinachoitwa "Marketing," Dunia sasa hivi inajua tayari kuwa tuna Tanzanite, lakini sisi tunashindwa kupenya kwenye soko," Katolila anaongezea.

"Huku Watanzania ambao wanatengeneza Tanzanite ni wengi sana. Lakini kwa ukweli Tanzanite huku kwetu inatoka kwa pesa ya kawaida, lakini tukipata soko ya nje tungekuwa tunaiuza kwa hela nyingi sana," anaongezea.

Tanzanite ina thamani kubwa ikiwa inaweza kuuzwa kati ya dola 100 na zaidi ya dola 500 kwa karati kulingana na ubora.

Ili kuilinda, serikali ya Tanzania imehimiza madini haya kuongezewa thamani ndani ya nchi kabla ya kuuzwa nje. Na pia imeweka mikakati ya kuhakikisha hakuna usafirishaji usio halali wa madini haya kutoka eneo la uchimbaji madini nchini humo.

"Ukiangalia hata nchi nyengine unapata sonara anatangaza katanzanite kadogo, amekanunua labda India au Thailand na unajiambia utaweza kuipata Tanzania kwa bei nafuu. Lakini watu wa Thailand wanafika wanaiuza Tanzanite kuliko vile wewe Mtanzania unavyoipata na kuitengeza licha ya kuwa iko nchini kwako unaweza kuiuza," Katolila anaelezea.

Ili kuilinda, serikali ya Tanzania imehimiza madini haya kuongezewa thamani ndani ya nchi kabla ya kuuzwa nje. Picha/others

Wataalamu wanashauri ongezeko la mauzo linafaa kuanzia nyumbani.

"Tunafaa tufike sehemu tujue vile tumebarikiwa kama nchi na tujivunie cha kwetu Natamani kila Mtanzania ikiwezekana kila Mtanzania awe na Tanzanite yake , iwe herini au pete, chochote. Kwasababu tayari tuna bahati kuwa nayo na kuipata kwa urahisi kuliko vile mtu mwingie anaweza kuipata , tungeanzia hapo na watu tusherehekee cha kwetu, " Katolila anasema.

Na pia kuna soko kubwa zaidi barani Afrika ambalo Tanzania inaweza kutumia madini ya Tanzania na kuyafanya kuwa fahari yake, kwani sekta ya urembo inazidi kukua hasa katika matumizi ya vifaa vya asili ya kiafrika.

TRT Afrika