Chama tawala nchini Tanzania (CCM) kimeiomba Wizara ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kuwaelekeza wasimamizi Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kupuuza makosa madogo madogo yaliyotokea, ili kuruhusu wagombea wengi kushiriki uchaguzi huo.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt Emmanuel John Nchimbi, ametoa mfano wa makosa ambayo yanapaswa kupuuzwa kuwa ni pamoja na wagombea kukosea herufi za majina.
Kwa mujibu wa Nchimbi, ni vyema kwa TAMISEMI kuangalia uwezekano wa kuwarudisha wagombea wote walioenguliwa kutokana na makosa hayo madogo madogo ili kuhamasisha ukuaji wa demokrasia kwenye uchaguzi huo.
Mara ya mwisho kwa Tanzania kufanya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ilikuwa ni Novemba 2019.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni hatua muhimu kwa Tanzania, wakati taifa hilo likijiandaa kufanya Uchaguzi Mkuu mwaka 2025.